Asilimia 75 ya Wafaransa hawataki Rais Hollande agombee tena urais
Robo tatu ya raia nchini Ufaransa wanapinga Rais wa nchi hiyo François Hollande kugombea tena urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ripoti iliyotolewa leo Alkhamisi na taasisi inayojishughulisha na ukusanyaji maoni ya YouGov nchini Ufaransa imeonyesha kuwa, asilimia 75 ya raia wa nchi hiyo wanapinga rais huyo kuwania tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa mwaka kesho 2017. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, kiwango cha mapenzi ya raia kwa Rais Hollande kimeendelea kushuka na kufikia asilimia 13 mwezi huu wa Aprili. Taasisi hiyo ya YouGov imesisitiza kuwa, asilimia 78 ya Wafaransa wanaona hatua ya rais huyo ya kutoifanyia marekebisho sheria ya kupokonya uraia, haikuwa sahihi. Aidha taasisi hiyo imeongeza kuwa, asilimia 70 ya raia wa nchi hiyo walioshiriki katika utoaji maoni wameonyesha kupinga pia hatua ya Manuel Valls, Waziri Mkuu wa Ufaransa ya kuunga mkono marekebisho ya sheria ya kazi, ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya taifa hilo. Hadi sasa serikali ya Kisosholisti nchini Ufaransa haijaweza kutatua matatizo ya kiuchumi iliyoahidi kuyatatua huko nyuma. Mbali na hayo, Ufaransa pia inakabiliwa na matatizo ya usalama yanayotokana na tishio la ugaidi ukiwemo pia mgogoro wa wahajiri barani Ulaya.