Matamshi dhidi ya hijabu ya Waziri Mkuu wa Ufaransa yazidi kulalamikiwa
Wito wa Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls wa kutaka vazi la hijabu lipigwe marufuku katika vyuo vikuu vya nchi hiyo limezusha makelele makali miongoni mwa mawaziri wa serikali.
Manuel Valls alisema katika mahojiano aliyofanya siku ya Jumanne na gazeti la nchi hiyo la Libération kama ninavyomnukuu:" Tunapaswa kuifanya kazi hii, lakini kuna sheria ndani ya Katiba ambazo zinatatiza upigaji marufuku huo".
Waziri Mkuu wa Ufaransa aidha amesema viongozi wa serikali na vyuo vikuu wanapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhusiana na kutekelezwa sheria za Usekulari katika ngazi ya Elimu ya Juu.
Aidha matamshi ya Manuel Valls, kwamba "raia walio wengi zaidi wa Ufaransa" wanahisi kuwa Uislamu unakinzana na thamani za Jamhuri ya Ufaransa yamewashangaza Waislamu wa nchi hiyo.
Matamshi hayo ya utatanishi ya Waziri Mkuu wa Ufaransa yamekabiliwa na upinzani mkali wa mawaziri wa serikali yake ya mrengo wa kati wa kushoto.
Waziri wa Elimu ya Juu Thierry Mandon, amesema hakuna haja ya kuwa na sheria kuhusu Hijabu katika vyuo vikuu na kuongeza kuwa wanachuo ni watu wazima, hivyo wana haki kamili ya kuwa na Hijabu; na kuvaa Hijabu si marufuku katika jamii ya Ufaransa.
Naye Waziri wa Elimu Najat Vallaud-Belkacem amesema anapinga hatua yoyote ya kupiga marufuku Hijabu katika vyuo vikuu vya serikali. Amefafanua kama ninavyomnukuu:"Wanachuo wengi wa kigeni wanasoma katika vyuo vikuu vyetu, je tunataka kuwakosesha masomo kwa sababu tu ya kuvaa aina ya mavazi inayohusiana na utamaduni wao?"
Ufaransa imeweka sheria kali zaidi dhidi ya uvaaji Hijabu katika maeneo ya umma miongoni mwa nchi za Ulaya.
Ikiwa na idadi kubwa zaidi ya Waislamu kati ya nchi za Ulaya, mnamo mwaka 2004 serikali ya Paris ilitangaza sheria ya kupiga marufuku wanafunzi wasichana Waislamu na hata mama zao kuingia shuleni wakiwa wamevaa vazi la heshima la Kiislamu la Hijabu.../