Mkuu wa CIA: Kuwekwa hadharani nyaraka ziitwazo 'kurasa 28' ni makosa
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i6214-mkuu_wa_cia_kuwekwa_hadharani_nyaraka_ziitwazo_'kurasa_28'_ni_makosa
Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA amesema itakuwa bora kama nyaraka za "kurasa 28" kuhusu tukio la Septemba 11 hazitowekwa hadharani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2016 23:43 UTC
  • Mkuu wa CIA: Kuwekwa hadharani nyaraka ziitwazo 'kurasa 28' ni makosa

Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA amesema itakuwa bora kama nyaraka za "kurasa 28" kuhusu tukio la Septemba 11 hazitowekwa hadharani.

John Brennan, ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya NBC na kueleza kwamba ni makosa kuziweka hadharani nyaraka za siri za kurasa 28 kuhusu tukio la Septemba 11, kwa sababu taarifa zake si za uhakika.

Brennan ameongeza kuwa taarifa zilizomo kwenye nyaraka za kurasa 28 hazijachunguzwa wala kuthibitishwa, kwa hivyo kuwekwa hadharani nyaraka hizo katika mazingira kama hayo kutawapa kisingizio wale wanaotaka kuihusisha Saudi Arabia na tukio la Septemba 11.

Kabla ya safari ya hivi karibuni ya Rais Barack Obama wa Marekani nchini Saudia, maafisa wa Ikulu ya White House na wa usalama walieleza bayana kuwa wanakusudia kuziweka hadharani nyaraka za siri zijulikanazo kama "kurasa 28". Kutolewa nyaraka hizo kunafichua uungaji mkono wa Saudia kwa watekaji nyara ndege waliohusika katika mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Akiwa nchini Saudia, Obama alifanya mazungumzo ya faragha juu ya suala hilo na mfalme Salman wa nchi hiyo. Baada ya safari hiyo ya Obama huko Saudia maelezo ya viongozi wa Washington kuhusu kutolewa nyaraka hizo yamebadilika kikamilifu.

Ikumbukwe kuwa Saudia ilitishia kwamba endapo nyaraka hizo zitawekwa hadharani itaondoa mitaji yake ya mabilioni ya dola katika benki za Marekani.../