Kinara wa Mapinduzi Mali atangaza baraza jipya la mawaziri
Kinara wa mapinduzi ya kijeshi Mali ametangaza serikali mpya yenye maafisa wa kijeshi.
Kanali Assimi Goita, ambaye aliongoza mapinduzi ya pili mwezi uliopita, ameteua mawaziri wapya ambapo wanajeshi wamepata nyadhifa muhimu.
Goita aliongoza mapinduzi ya mwezi Agosti mwaka jana, wakati yeye na maafisa wengine wa jeshi walipomwondoa mamlakani rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita baada ya maandamano ya wiki kadhaa juu ya ufisadi na mzozo wa muda mrefu wa magaidi wakufurishaji
Baada ya Jumuiya ya Afrika Magharibi ya ECOWAS kumshinikiza, mamlaka ya kijeshi ilikabidhi madaraka kwa serikali ya mpito inayoongozwa na raia, lakini Goita aliwapindua tena viongozi hao mnamo Mei 24. Katika tukio hilo wanajeshi nchini Mali walimkamata rais na waziri mkuu wa serikali ya mpito iliyoundwa baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi ya Agosti mwaka uliopita.

Maafisa wa jeshi waliwaachia viongozi hao siku kadhaa baadaye, lakini walitangaza kuwavua madaraka yao katika mkasa uliozusha lawama kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Afrika umetangaza kusimamisha uanachama wa Mali, ikiwa ni jibu kwa hatua ya jeshi la nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito.
Benki ya Dunia pia imesimamisha shughuli zake za kifedha nchini Mali na kusema kuwa inafuatilia kwa karibu matukio na hatua zinazochukuliwa huko nchini Mali.