Muqawama wa Palestina wawapongeza wananchi wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101592
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa shukrani rasmi kwa wananchi wa LIbya kwa hatua yao ya kuonesha msimamo imara wa kulaani hatua ya waziri wa mambo ya nje wa Libya ya kuonana na waziri wa mambo ya nje wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 29, 2023 02:45 UTC
  • Muqawama wa Palestina wawapongeza wananchi wa Libya

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa shukrani rasmi kwa wananchi wa LIbya kwa hatua yao ya kuonesha msimamo imara wa kulaani hatua ya waziri wa mambo ya nje wa Libya ya kuonana na waziri wa mambo ya nje wa Israel.

Siku ya Jumapili, televisheni ya utawala wa Kizayuni ilitangaza kuwa, waziri wa mambo ya nje wa Israel, Eli Cohen ameonana na waziri wa mambo ya nje wa Libya, Najla al Mangoush nchini Italia.

Mara baada ya kuenea taarifa hiyo, Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid al Dbeibeh, alimsimamisha kazi Mangoush na waziri huyo wa mambo ya nje wa Libya amekimbilia nchini Uturuki. 

Wananchi wa Libya wachoma moto bendera ya utawala wa Kizayuni

Vyombo vya habari vya Palestina vimemnukuu Hazem Qasim, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS akisema jana Jumatatu kwamba, upinzani mkali uliooneshwa na wananchi wa Libya dhidi ya kitendo hicho cha Najla al Mangoush unaonesha dhati ya wananchi wa Libya ya kuunga mkono kadhia ya Palestina ambalo ndilo suala muhimu zaidi katika umma mzima wa Kiarabu na Kiislamu. Upinzani huo umethibitisha kivitendo kuwa utawala wa Kizayuni ndiye adui mkuu wa umma, tangu zamani, hivi sasa na milele.

Msemaji huyo wa HAMAS pia amewataka wananchi wa nchi zote za Kiarabu na Kiislamu kupinga vikali na kwa nguvu zote jaribio lolote la kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel. Amesisitiza kuwa, kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kunatoa pigo kwa manufaa ya kitaifa ya nchi husika na ni hatari kubwa kwa kadhia ya Palestina.

Mara baada ya kutangazwa habari ya kuonana mawaziri hao wawili wa Libya na Israel, wananchi wenye hasira wa Libya wamefanya maandamano na kuchoma moto bendera za utawala wa Kizayuni katika miji ya Zawiya na Tajoura.