Kuchukiwa utawala haramu wa Israel na wananchi wa ulimwengu wa Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101612-kuchukiwa_utawala_haramu_wa_israel_na_wananchi_wa_ulimwengu_wa_kiarabu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Libya, Najla al Mangoush amekimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi kwa kosa la kuonana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni nchini Italia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 29, 2023 05:37 UTC
  • Kuchukiwa utawala haramu wa Israel na wananchi wa ulimwengu wa Kiarabu

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Libya, Najla al Mangoush amekimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi kwa kosa la kuonana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni nchini Italia.

Hayo ni kwa mujibu wa televisheni ya WION ambayo imesema kwamba, al Mangoush amekiri kuwa alifanya mazungumzo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel kwa uratibu wa Antonio Tajani Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, lakini amedai kuwa mazungumzo hayo hayakuwa rasmi na hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa.

Hata hivyo utawala wa Kizayuni unachukiza mno katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kiasi kwamba, kitendo chochote cha kuwa karibu na Wazayuni kinapokewa kwa hasira kubwa.

Kilichotokea Libya kwa mara nyingine tena kimesawiri na kuonyesha taswira ya hasira, ghadhabu na chuki za wananchi wa eneo la Magharibi mwa Asia na Kaskazini mwa Afrika dhidi ya utawala haramu wa Israel unaoukalia kwa mabavu wa Quds tukufu. Hasira hii ni kubwa kiasi kwamba hata kikao cha afisa wa Libya katika kikao kisicho rasmi na kisichopangwa na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni hakikubaliki, na Najla Al-Mangoush amelipa gharama ya hilo kwa kusimamishwa kazi na badaye kuikimbia nchi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala ghasibu wa Israel Eli Cohen Jumapili ya juzi alitoa habari ya kukutana na kuzungumza na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Libya Bi Najla Al-Mangoush na kusema kuwa mkutano huo ulifanyika wiki iliyopita huko Roma, mji mkuu wa Italia. Aliutaja mkutano huu kuwa wa kihistoria.

Saa chache tu baada ya kutangazwa kwa habari hiyo, wananchi wa Libya walifanya maandamano makubwa na kulaani mkutano wa Najla Al-Mangoush na Eli Cohen.

Katika kuonyesha hasira zao dhidi ya serikali baada ya waziri wa mambo ya nje wa Libya kuonana na waziri huyo Mzayuni, wananchi waliokuwa na hasira wa Libya wamechoma moto bendera ya Israel na kulaani kitendo chochote cha kuwa karibu na utawala katili wa Israel

Katika mji wa mashariki mwa Libya wa Tajoura, waandamanaji walifunga barabara kuu kulalamikia kitendo cha Najla al Mangoush cha kukutana na Mzayuni huyo na kuapa kuendeleza maandamano yao ikiwa ni pamoja na kufunga njia ya reli kuelekea makao makuu ya serikali ya Waziri Mkuu Abdul Hamid al-Dbeibeh kama hatua kali hazitachukuliwa dhidi ya Najla. Watumiaji wa mitandao ya kijami pia nchini Libya wamelaani mkutano huo na kuuita kuwa ni usailiti na uhaini. Chama cha Uadilifu na Ujenzi cha Libya kimesisitiza katika taarifa yake kwamba, hatua hii ya hatari ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa.

Maandamano ya kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel

Baada ya kushadidi maandamano na hasira za wananchi na baadhi ya makundi ya kisiasa, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ilitangaza katika taarifa yake kwamba imemsimamisha kazi Waziri huyo wa Mashauri ya Kigeni kutokana na kukutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni mjini Roma na kupeleka jina lake kwenye taasisi za ufuatiliaji uchunguzi.

Kabla ya hapo pia kumeshuhudiwa pia wimbi la chuki mara chungu nzima dhidi ya Israel.

Moja ya yaliyokuwa matukio ya kuvutia katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar ni kukataa wananchi wa mataifa mbalimbali ya Kiarabu kuhojiwa na vyombo vya habari vya Israel na vilevile kuiunga mkono Palestina dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.

Katika mashindano hayo, watazamaji wa kutoka Qatar, Tunisia, Lebanon na hata Saudi Arabia walikataa kuhojiwa na waandishi wa habari wa Israel. Wakati timu yao inapocheza, watazamaji kutoka Tunisia na Morocco walikuwa wakibeba na kuonyesha mabango ya kuunga mkono Palestina, suala ambalo lilikuwa la dhahir shahir mpaka vyombo vya habari vya Israel na Magharibi vililazimika kuliakisi. Mbali na hayo, baadhi ya watazamaji walikuwa na bendera za Palestina na hata wakati mwingine kupiga nara za kuliunga mkono taifa la Palestina.

Bila ya shaka sababu ya kuchukiwa huko ni uvamizi, ubaguzi wa rangi na ukatili wa kupindukia unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Utawala wa Kizayuni ambao ni dola bandia katika eneo la Magharibi mwa Asia na umezikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, unaendeleza uvamizi huo kwa kunyakua ardhi na nyumba za Wapalestina na kuwatimua wananchi hao madhulumu kutoka katika nyuma na makazi yao. Ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ni mfano na kielelezo cha wazi cha siasa hizo za Israel.

Wakati wa kombe la Dunia Qatar mwaka jana (2022) kulishuhudiwa uungaji mkono mkubwa kwa Palestina na kuonyeshwa chuki dhidi ya Israel

 

Fauka ya hayo, ubaguzi wa rangi uko katika dhati na asili ya utawala huo katili. Baraza la sasa la mawaziri la Israel linaloongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kama walivyokiri Wazayuni wenyewe ni kuwa, ndilo baraza la mawaziri waliokithirisha zaidi vitendo vya kibaguzi.

Uvamizi wa mara kwa mara wa baadhi ya mawaziri katika Msikiti wa Al-Aqswa na kufukuzwa waumini wa Kipalestina kutoka katika eneo la msikiti huo mtakatifu ni mifano ya ubaguzi wa kimfumo wa utawala wa Kizayuni. Ukandamizaji wa kupindukia dhidi ya Wapalestina hususan wanawake na watoto na kuuawa shahidi na kujeruhiwa kila siku wananchi wa Palestina ni sababu nyingine muhimu ya kukithiri kwa chuki za wananchi katika eneo la Magharibi mwa Asia dhidi ya utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds tukufu.

Nukta ya mwisho ni kuwa, hasira ya watu wa Libya kwa mkutano wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo na mwenzake wa Kizayuni na kusimamishwa kazi kwa afisa huyo wa Libya na kisha kuikimbilia, imethibitisha kwa mara nyingine tena kwamba, harakati za kurejesha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zimeshindwa na kugonga mwamba haraka mno na hazijawa na matokeo ya kuridhisha yaliyokuwa yakitarajiwa na viongozi wa Tel Aviv.