Lebanon katika mkwamo wa kumchagua Rais mpya
Licha ya Bunge la Lebanon kufanya zaidi ya vikao 10 kwa ajili ya kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo, lakini hadi sasa limeshindwa kumpata Rais na hivyo kupelekea mkwamo wa kumchagua kiongozi wa juu zaidi nchini humo kuendelea kushuhudiwa.
Karibu mwaka mmoja sasa tangu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Michel Aoun amalize muda wake.
Wabunge wa Lebanon wamekutana zaidi ya mara kumi katika vikao vilivyoitishwa maalumu kwa ajili ya kumchagua Rais lakini wameshindwa kumpata rais kutokana na sababu kuu mbili.
Sababu ya kwanza ni kutotimia baadhi ya vikao idadi inayotakiwa ya wabunge ili kikao kifanyike na sababu ya pili ni kushindwa kupata kura zinazohitajika wagombea waliojitokeza kuwania kiti cha urais.
Muhula wa urais wa rais wa sasa wa Lebanon Michel Aoun, ulimalizika tangu tarehe 31 Oktoba mwaka jana; na kushindwa kumchagua rais mpya kunashadidisha mgogoro wa ombwe la kisiasa la nchi hiyo kubaki bila ya rais.
Bunge la Lebanon linapaswa kumchagua Rais mpya mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Rais aliyeko madarakani. Aidha kwa mujibu wa katiba, Rais wa nchi anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Kimaroni.
Kutumbukia Lebanon katika mkwamo wa kushindwa kumchagua Rais mpya kunaifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuzidi kuwa tete sambamba na kuongeza matatizo ya kiuchumi ambayo tayari yanaiandama nchi hiyo hivi sasa.
Kuna hitilafu kubwa kuhusiana na wagombea urais. Kile ambacho kimetokea hadi sasa katika vikao vya Bunge kinaonyesha kuwa, hakuna azma na dhamira ya dhati kwa ajili ya kumchagua Rais. Kuna mpasuko mkubwa baina ya makundi na mirengo ya kisiasa nchini Lebanon hasa kwa kuzingatia kwamba, baadhi ya mirengo na vyama vinafanya juhudi kuhakikisha kwamba, Rais ajaye anatoka katika kambi inayoipinga Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Kwa mujibu wa makubaliano makongwe ya kisiasa nchini Lebanon, cheo cha Rais kinapaswa kushikiliwa na Wakristo, Waziri Mkuu anapaswa kuteuliwa kutokka miongoni mwa Waislamu wa Kisuni na Spika wa Bunge anapaswa kutoka miongoni mwa Waislamu wa Kishia.
Hali hii ambayo ilifikiwa baada ya hati ya makubaliano ya amani ya Taif mwaka 1989 ambayo ilikubaliwa na mirengo na makundi yote ya kisiasa nchini Lebanon imegeuka na kuwa msingi wa uthabiti. Kikawaida kuchaguliwa Spika wa Bunge huwa jambo jepesi hasa kwa kuzingatia kukubalika Nabih Berri. Lakini kibarua kigumu na msuguano mkali hujitokeza katika kuchagua Rais na hata Waziri Mkuu.
Sababu ya kwanza ya mkwamo wa kuchaguliwa Rais ni kuweko hitilafu ndani ya Wakristo wa Kimaroni wenyewe ambao kimsingi wanapaswa kupendekeza majina ya wagombea ambao huwasilishwa Bungeni na kupigiwa kura. Hali si shwari baina yao kwani hawajafikia kauli moja kuhusiana na mgombea fulani.
Sababu nyingine ni kutokuweko mtazamo mmoja baina ya makundi ya kisiasa ya Lebanon kuhusiana na mgombea fulani ili yaweze kumpigia kura na hivyo kumfanya aibuke na ushindi hasa kwa kuzingatia kwamba, hakuna mrengo wenye wingi mutlaki katika Bunge la Lebanon.
Kwa sasa serikali ya Lebanon inaongozwa na serikali kishikizo na ili kuchagua Waziri Mkuu mpya ni lazima achaguliwe kwanza Rais ambaye ndiye atakayemteua Waziri Mkuu na kumpa jukumu la kuunda serikali baada ya Waziri Mkuu huyo kupigiwa kura Bungeni ya kuwa na imani naye.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kile ambacho kinaelezwa kuwa "demokrasia ya kijamii" kivitendo ni uwiano wa nguvu za kikaum nchini Lebanon.
Licha ya kuwa katika miaka ya nyuma imewahi kuelezwa mara kadhaa kwamba, sababu kuu ya mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon ni hitilafu baina ya Saudi Arabia na Iran, lakini hivi sasa hata baada ya kupatana Riyadh na Tehran hakujapatikana faraja katika kulipatia ufumbuzi ombwe la Rais nchini Lebanon.
Sababu za ndani zinazosababishwa na hitilafu kati ya pande tofauti zimesababisha Walebanon kuendelea kusubiri matukio ya nje, ya kieneo na ya kimataifa ili kulifanya faili la Rais kuwa amilifu.
Huko nyuma, uwepo na ushawishi wa makundi ya kigeni nchini Lebanon ulikuwa ukitajwa kuwa sababu ya mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon ambapo kuchaguliwa Rais kulikuwa kukitegemea kuweko maafikiano ya kieneo na kimataifa juu ya mgombea fulani. Lakini hii leo hali ya mambo nchini Lebanon haiko hivyo na bila shaka, kufikia mwafaka na makubaliano ya ndani ni jambo muhimu zaidi na njia ya kwanza muhimu ya kuindoa nchi hiyo katika mkwamo wa kuchagua Rais na kwa muktadha huo kuhitimisha ombwe la uongozi nchini humo