Duru mpya ya migawanyiko ya ndani katika utawala haramu wa Israeli
Baada ya mzozo wa ndani wa utawala wa Kizayuni Israel uliosababishwa na mpango tata wa mabadiko ya sheria za mahakama ambao umependekezwa na waziri mkuu, Benjamin Netanyahu, na maandamano makubwa ya kupinga mpango huo, sasa mshtuko mpya ambao haujawahi kutokea umeigubika jamii ya Kizayuni.
Ghasia za kushtua zilitokea Jumamosi mjini Tel Aviv na kudhihirisha sura nyingine za migawanyiko ya ndani ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Ghasia hizo zilizokuwa na umwagaji damu, zilitokea kati ya vikosi vya polisi vya utawala dhalimu wa Israel na wahamiaji wenye asili ya Afrika, haswa Waeritrea na Wasudan, ambapo karibu watu 200 walijeruhiwa kutoka pande zote mbili.
Afisa mkuu wa polisi aliliambia gazeti la Kizayuni la Haaretz kwamba: "Maafisa wa polisi hawakuwa tayari kukabiliana na kiwango hiki cha machafuko, na tumeona kiwango hiki cha mzozo hapo awali katika Ukingo wa Magharibi, lakini hali kama hii haijawahi kutokea Tel Aviv."
Duru za Kizayuni zimedai kuwa, chanzo cha migogoro hiyo ni makabiliano kati ya wapinzani na waungaji mkono wa Rais wa Eritrea, na kwa njia hiyo walijaribu kuficha mifarakano ya ndani kati ya serikali ya Kizayuni, hasa baraza la mawaziri lenye misimamo mikali ya kibaguzi la Netanyahu, na Mayahudi wenye asili ya Afrika.
Lakini ushahidi uliopo unaonyesho kuwa, kuna agizo la dharura la baraza la mawaziri la Netanyahu la kuwatimua Mayahudi wenye asili ya Afrika ambao walishiriki katika ghasi za Jumamosi, na jambo hili inaonyesha kwamba serikali ya kibaguzi iliyoko madarakani Tel Aviv ilikuwa inasubiri fursa ya kuchukua hatua dhidi ya watu hao wenye asili ya Afrika.
Chini ya siku moja baada ya maandamano makubwa ya watu wenye asili ya Afrika kutoka Eritrea mjini Tel Aviv, baraza la mawaziri la Netanyahu limeunda kamati maalumu ya mawaziri ambayo kazi yake ni kuchunguza uwezekano wa kuwafukuza waandamanaji hao Waafrika. Kamati hiyo iliundwa baada ya Itamar Ben-Gvir, waziri wa mambo ya ndani wa utawala wa Kizayuni, kumtaka Netanyahu awaruhusu polisi kukabiliana na waandamanaji wa Eritrea na kisha kuwafukuza.
Huko nyuma, ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya Wapalestina ambao ni wakazi asili wa ardhi zlizopachikwa jina la Israel pia baada ya kupungua wahajiri wa Kiyahudi kutoka nchi nyengine, utawala wa Kizayuni uliamua kuwaleta Mayahudi wenye asili ya Kiafrika. Lakini hivi sasa wanasiasa Wazayuni wenye misimamo mikali ya kibaguzi katika baraza la mawaziri la Netanyahu, hawawataki tena Mayahudi hawa wenye asili ya Afrika. Hii ni kwa sababu, marabi au makuhani wa Kiyahudi walio na ushawishi katika baraza la mawaziri la Netanyahu, hawatambui hata kidogo utambulisho wa Kiyahudi wa wahamiaji wenye asili ya Afrika.
Si muda mrefu uliopita, mmoja wa makuhani wakuu wa Israeli aliwaita watu weusi au wenye asili ya Afrika kuwa eti ni nyani, na ingawa alikosolewa kama "mbaguzi wa rangi", lakini hakuwahi kushtakiwa kwa maoni yake ya kibaguzi wala hakuomba msamaha.
Hivi sasa kuwatimua Waafrika ni katika ajenda nzito ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na ikiwa huko nyuma utawala huu ulijaribu kuwahimiza kurejea katika nchi yao au nchi nyingine yoyote kwa kutumia baadhi ya motisha, lakini sasa kwa kutumia fursa iliyotokana na ghasia, itawalazimu Waafrika hao kuondoka.
Ingawa maandamano ya watu wenye asili ya Afrika ya hivi majuzi mjini Tel Aviv yalichochewa na kisingizio cha kupinga sherehe iliyofanyika katika ubalozi wa Eritrea mjini Tel Aviv, lakini kujiunga Waafrika wengine weusi wakiwemo Wasudan katika maandamano dhidi ya serikali ya Netanyahu kulionyesha kuwa jamii ya Wazayuni weusi ilikuwa ikingoja cheche ili kupinga ubaguzi wa rangi ambao umekita mizizi kitaasisi katika jamii ya Kizayuni.
Kulingana na Sharon Abraham Weiss, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki za Kiraia la Tel Aviv, "katika Israeli, kuna uwezekano mkubwa wa kukiukwa haki za watu weusi, na watu weusi walio chini ya umri wa miaka 18 wana uwezekano wa kufungwa gerezani mara nne zaidi kuliko wenzao weupe."
Takwimu zinaonyesha kuwa, thuluthi moja ya vijana 200 katika magereza ya Israel ni Waethiopia, wakati Wayahudi 126,000 wenye asili ya Ethiopia ni asilimia mbili tu ya wakazi wa Israel.
Ubaguzi ulioshamiri dhidi ya wahajiri wenye asili ya Kiafrika umewapelekea kujitokeza mitaani kuandamana wakilalamikia ubaguzi wa rangi katika utawala wa Kizayuni.
Katika kipindi cha muongo moja uliopita, Israel imekabiliwa na maandamano saba makubwa ya watu weusi au wenye asili ya Afrika ambao wanalalamikia ubaguzi wa rangi. Kwa maneno mengine ni kuwa, kila baada ya miezi 18, jamii ya Kizayuni inakabiliwa na vuguvugu la maandamano ya watu weusi, na kwa maana hii, ingawa mapigano ya Jumamosi huko Tel Aviv hayakuwa ya kawaida, lakini hayajawahi kutokea kwa ukubwa kama huo.
Maandamano hayo ya Waafrika wanaopinga ubaguzi mjini Tel Aviv ni jambo linalofichua mwelekeo mpya wa migawanyiko ya ndani ya Israel, pamoja na mtazamo wa kibaguzi wa baraza la mawaziri lenye msimamo mkali la Netanyahu dhidi ya wahajiri wenye asili ya Afrika.