Jumbe za kisiasa za matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein
Kwa miaka kadhaa sasa, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali (as) yanafanyika kwa njia mpya na ya kupendeza zaidi kuliko nyakati zote za huko nyuma. Matembezi haya yana jumbe kadhaa za kisiasa.
Moja ya jumbe muhimu za kisiasa za matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein ni kutumia vyema diplomasia ya watu na mataifa. Hapana shaka yoyote kwamba, haiwezekani kwa serikali ya Iraq kufanya matembelezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) yanayoshirikisha zaidi ya watu milioni 20 peke yake, lakini Wairaqi na wasio Wairaqi, wote wanashiriki katika kusimamia na kufanya matembezi hayo makubwa na ya aina yake. Watu wote, bila ya kujali utaifa wao, wana nafasi katika kufanikisha shughuli hiyo ya kidini, japokuwa ni kweli kwamba taifa la Iraq ndilo lenye nafasi kubwa zaidi katika kadhia hii.
Katika diplomasia ya mataifa, watu wa nchi mbili au zaidi huhusika moja kwa moja na kujenga mawasiliano baina yao kwa mchango mdogo tu wa serikali. Katika aina hii ya udiplomasia, mwingiliano wa watu na mataifa tofauti hujenga mfungamano mkubwa ambao huwa vigumu kwa diplomasia rasmi kuweza kuutengeneza.
Ujumbe mwingine muhimu wa kisiasa wa Arubaini ya Imam Hussein ni kukurubiana zaidi kunakojitokeza baina ya serikali za nchi mbalimbali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, matembezi ya Arubaini ni jambo la kitamaduni na kidini. Kwa mfano tu katika miaka ya hivi karibuni, tumeona jinsi shughuli hiyo ya matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ilivyozidisha na kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kidini kati ya serikali mbili za Iraq na Iran. Kwa msingi huo, Arubaini ya Imam Hussein inazikurubisha pamoja pia serikali, kama ilivyo kwa watu na mataifa ya nchi tofauti.
Mojawapo ya jumbe muhimu za kisiasa za Arubaini ya Imam Hussein ni kuimarisha fikra ya mapambano na muqawama baina ya mataifa ya Kiislamu. Matembezi ya Arubaini yanayoshirikisha idadi kubwa ya watu yanaweza kuonekana kama dhihirisho kamili la diplomasia ya wananchi ya kambi ya muqawama. Kwa Baraka za fikra ya Arubaini ya Imam Hussein na mchango wa makamanda waliouawa shahidi wa muqawama, mataifa mawili ya Iran na Iraq yamekuwa katika safu moja kwa miaka kadhaa na yamefanya jitihada kubwa za kutokomeza makundi ya kitakfiri na kuimarisha fikra ya muqawama na mapambano dhidi ya dhulma na madhalimu.
Hili ni ndilo suala ambalo lilisisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei hapo awali akisema: "Iwapo mataifa ya nchi za Kiislamu yatakuwa na mwelekeo jumla kwenye masuala muhimu na makuu, Ulimwengu wa Kiislamu utafikia kilele cha maendeleo na ustawi. Popote pale tunaposhuhudia mifano ya mjumuiko huu, walau wa kimiili peke, mwangwi wake pia umeshuhudiwa duniani katika sura ya heshima na izza kwa Uislamu na Waislamu.”
Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) pia yanadhihirisha sura ya rehma, upendo na muawana ya Uislamu. Zaidi ya Waislamu milioni 20 wanaokwenda kumzuru Imam Hussein kutoka nchi mbalimbali, hushiriki katika matembezi ya Arubaini, lakini wakati huo hakushuhudiwi vurugu hata kidogo, na shughuli hiyo hufanyika kwa heshima, mshikamano, upendo na muawana, sambamba na kujitenga na masuala kimaada.
Shughuli ya matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) imethibitisha wazi kuwa, Al-Qaida, Boko Haram, Daesh, Taliban, n.k. si nembo za Uislamu na Waislamu. Fikra za Daesh hazina nafasi katika Ulimwengu wa Kiislamu, bali ni mawazo ambayo nchi za Magharibi zinataka yatambuliwe kama nembo na alama ya Uislamu. Kinyume chake, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) na ibada ya Hajj vinadhihirisha sura halisi ya Uislamu.