Matukio mapya ya kuzingatiwa nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101994-matukio_mapya_ya_kuzingatiwa_nchini_yemen
Safari ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Aden badala ya Sana'a imezua maswali mengi kuhusu malengo hasa ya safari hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2023 04:47 UTC
  • Matukio mapya ya kuzingatiwa nchini Yemen

Safari ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Aden badala ya Sana'a imezua maswali mengi kuhusu malengo hasa ya safari hiyo.

Jassim Mohammad al-Budaiwi, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi alikwenda Yemen siku ya Alkhamisi kwa mara ya kwanza tangu kuanza vita vya Yemen, yaani baada ya miaka minane, na kukaribishwa na Baraza la Urais lililo na mafungamano ya kisiasa na nchi za kigeni. Baraza la Urais la Yemen linaloongozwa na Rashad al Alimi lina uhusiano wa karibu sana na Riyadh na lilichukua nafasi ya serikali ya Mansour Hadi katika tukio lililofanana na mapinduzi tarehe 7 Aprili 2022.

Safari hiyo imefanyika katika mazingira ambayo Saudi Arabia inatekeleza mradi unaoitwa "Uwezeshaji wa Majimbo ya Yemen", ambao wenyewe unatiliwa shaka nyingi. Inasemekana kuwa kupitia mradi huo, Saudi Arabia inakusudia kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na majimbo ambayo hayako chini ya udhibiti wa Harakati ya Ansarullah.

Mradi huo ambao uko mbioni kutekelezwa kwa kisingizio cha kuwezesha serikali za mitaa, utachunguza pia changamoto zilizopo katika mikoa mbalimbali ya Yemen. Wakati wa kuchunguza rasilimali za ndani, si kwamba ni vyanzo vya mafuta pekee ndivyo vitajadiliwa bali pia uwezo wa mikoa ya pwani katika kubuni ajira na kudhaminiwa fedha kupitia uvuvi na kilimo katika mikoa mingine.

Manowari ya Marekani katika pwani ya Yemen

Misingi ya kwanza ya mradi huo itazingatia ushirikiano wa taasisi za serikali na pia kuhimiza sekta binafsi kushirikiana na serikali za mitaa. Baada ya kutekelezwa na kufanikiwa katika mikoa mitatu, mradi huo utatekelezwa katika mikoa mingine ya Yemen, na kwa mujibu wa watekelezaji wa mradi huo, mwishowe Yemen itatawaliwa kimajimbo kama ilivyo Marekani. Mpango huo unakumbusha mpango mwingine kama huo uliopendekezwa kabla ya kuanza vita huko Yemen, ambao ulipingwa vikali na wanamapinduzi na hatimaye kuwa sababu ya kuanza uvamizi wa kijeshi wa muungano wa Saudia dhidi ya watu wa Yemen.

Kuwasilishwa mpango huo sambamba na kuanza safari ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Aden badala ya Sana'a kumeambatana pia na matukio mengine kadhaa, ambayo kila moja linaweza kufichua sehemu ya malengo fiche ambayo yanafuatiliwa na watekelezaji wa mpango huo:

Jambo la kwanza ni kuwa, licha ya kuboreka uhusiano wa kisiasa wa Iran na Saudi Arabia, lakini bado hakujawa na uwazi katika utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Yemen. Mgogoro wa Yemen haujapatiwa ufumbuzi wowote hadi sasa licha ya juhudi kubwa ambazo zimefanyika katika uwanja huo, hasa katika miezi mitatu iliyopita. Hatua pekee iliyopigwa kuhusu suala hilo ni meli ya mafuta ya “Safar” ambayo mafuta yake yamepakuliwa na hivyo kuondolewa hatari ya kumwagika mafuta hayo baharini na kuchafuliwa mazingira.

Ingawa, Aprili iliyopita, jumbe mbili za wawakilishi kutoka Saudi Arabia na Oman zilianza mazungumzo na viongozi wa Ansarullah huko Sana'a, ambayo yalidumu kwa siku 6 kwa ajili ya kuchunguza njia za kurefusha usitishaji vita na kuanzisha mkondo wa amani nchini Yemen, lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote ya maana yaliyopatikana katika uwanja huo.

Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi

La pili ni kwamba nafasi ya Marekani katika vita vya Yemen imeongezeka sana katika wiki za hivi karibuni, jambo ambalo limepelekea Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, inayoongozwa na Ansarullah, kuonya mara kadhaa dhidi ya harakati mpya za jeshi la Marekani katika mwambao wa nchi hiyo. Baada ya kuongezeka maonyo ya viongozi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa kuhusu mienendo ya kutia shaka ya Marekani, Bunge la Yemen pia limetoa tamko, likilaani vikali harakati za kijeshi zinazotiliwa shaka za Marekani katika eneo la mashariki na majimbo ya kusini pamoja na hatua ya askari wa Marekani ya kuingia katika shule kadhaa katika mkoa wa Hadhramaut mashariki mwa Yemen. Tamko hilo linasema: Maonyo ya Seyyed Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi kiongozi wa Harakati ya Ansarullah na Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen yanapaswa kupewa uzito unaostahiki na kupuuzwa matakwa ya kiadilifu na halali ya taifa la Yemen na kutoyatekeleza, hasa katika hali ambayo Yemen ina irada na nguvu za kutosha, kunaipa nchi hii ruhusa ya kuchukua hatua za kutetea haki zake halali.

Jambo la tatu ni kuwa, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa Marekani imeongeza tena hatua zake za kutoa adhabu jumla kwa watu wa Yemen kutokana na mapambano ya serikali yao dhidi ya matakwa ya kibeberu ya nchi hiyo ya Magharibi. LIicha ya ukweli kwamba kwa sasa mamilioni ya Wayemen wanahitaji msaada wa dharura wa chakula, lakini Mpango wa Chakula Duniani WFP uko chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani kwa ajili ya kupunguza misaada yake kwa watu hao masikini.