Misri yafungua tena kivuko cha Rafah kwa muda
Misri imefungua tena kivuko cha Rafah, njia pekee inayotumiwa kufikishia misaada ya dharura kwa Wapalestina karibu milioni mbili walio chini ya mzingiro huko Ukanda Gaza tangu mwaka 2007 na kusema kuwa eneo hilo la mpakani litasalia wazi hadi Julai 4.
Taarifa kutoka Cairo zinasema kuwa, kivuko hicho kimefunguliwa kuanzia leo Jumatano hadi Julai 4, lakini kitafungwa Ijumaa ya Julai Mosi. Zaidi ya Wapalestina 3,000 waliondoka Ukanda wa Gaza wakati kivuko cha Rafah kilipofunguliwa tena na Misri kwa muda wa siku nne, katika wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Juni, kabla ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani. Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema katika mwaka 2015, kivuko cha Rafah kilifunguliwa kwa muda wa siku 21 tu na hivyo kuufanya mwaka huo kuwa mbaya zaidi kwa watu wa Gaza. Mahmoud al-Zahar, Kiongozi mwandamizi wa Hamas amesema wana matumaini ya kufunguliwa moja kwa moja kivuko cha Rafah ambacho ni kivuko muhimu zaidi kinachounganisha eneo la Ukanda wa Gaza, Palestina na ulimwengu wa nje. Hali ya Wapalestina wa Gaza imekuwa mbaya zaidi baada ya jeshi kumtimua madarakani rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Mohammad Morsi mnamo Julai 2013. Mtawala wa sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi, ambaye alikuwa mkuu wa jeshi wakati wa kupinduliwa Morsi, amekuwa akishirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwakandamiza Wapalestina huko Ghaza.