Operesheni yenye maafa makubwa ya Netanyahu huko Gaza
Utawala wa Kizayuni na Baraza la Mawaziri lenye misimamo mikali na amblo pia ni la mrengo wa kulia la Netanyahu linatekeleza mashambulizi mauaji makubwa na ya kijinai huko Ghaza.
Katika wiki moja iliyopita, tangu kupata kipigo cha Kimbunga cha Al Aqsa, utawala wa Kizayuni na Baraza la Mawaziri la Netanyahu lenye msimamo mkali, limewaua shahidi na kuwajeruhi zaidi ya raia 10,000, wengi wao wakiwa ni watoto, vijana na wanawake. Kwa kuzingatia kuwa jeshi la Kizayuni linashambulia kwa makusudi vituo vya matibabu na hospitali ili kuwahamisha watu wa Ghaza, na hadi sasa limeshalenga zaidi ya vituo 20 vya matibabu na makumi ya waokoaji, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka idadi ya mashahidi kutokana na idadi kubwa ya majeruhi na kukosekana vifaa vya matibabu na kufungwa kwa vituo vingi vya afya na tiba. Vilevile, wakati wa mashambulizi ya kipofu ya anga ya utawala wa Kizayuni, zaidi ya wakaazi laki nne wa Ghaza wamelazimika kuyahama makaazi yao na kuwa wakimbizi katika maeneo mengine, na hii ni pamoja na kuwa utawala huo umetoa muda kwa zaidi ya wakazi milioni moja wa kaskazini mwa Ghaza kuondoka makwao mara moja, jambo ambalo linaongeza uwezekano wa kutekelezwa hivi karibuni shambulio la nchi kavu katika eneo hilo.
Awali, ilidhaniwa kuwa mateka wa Israel walioko mikononi mwa Hamas wangekuwa kikwazo dhidi ya mashambulizi ya kipofu na kinyama katika Ukanda wa Ghaza, lakini sasa ni wazi kwamba Netanyahu na Baraza lake la mawaziri lenye misimamo mikali na la mrengo wa kulia hawajali hata maisha ya mateka wao wanaoshikiliwa huko Ghaza na mashambulizi hayo ya anga yamepelekea kuuawa zaidi ya mateka 10 wa utawala huo.
Ingawa inawezekana kwamba suala hilo halitafuatiliwa wakati wa vita vya Gaza, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba baada ya kumalizika vita, kushindwa kuokoa maisha ya mateka wa Israel kutaongezwa katika kesi zinazomkabili Netanyahu katika mahakama za utawala huo na hivyo kuongeza wigo wa upinzani wa ndani dhidi yake.
Ikiwa kabla ya hapo, mswada unaojulikana kama mageuzi ya mahakama, ambayo wapinzani wametafsiri kama mapinduzi ya mahakama, ulichukuliwa kuwa suala muhimu zaidi la mzozo wa ndani, bila shaka baada ya kumalizika vita vya Ghaza, kuchelewa na kushindwa kuokolewa mateka wa Israel kutazusha mzozo mpya na kueneza wigo wa mivutano ya kisiasa ndani ya utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Suala hilo pia linaweza kuongeza tofauti za ndani kati ya jeshi na Baraza la Mawaziri la Netanyahu. Inapozingatiwa kwamba wakati wa mageuzi ya mahakama, jeshi lilichukua upande wa upinzani na kuungana na waandamanaji, inawezekana kwamba askari wa jeshi watakuwa na dhana kwamba Netanyahu na baraza lake la mawaziri watalituhumu jeshi kuwa lilishindwa kuokoa maisha ya mateka.
Siasa za itikadi kali za Baraza la Mawaziri la mrengo wa kulia, pamoja na kuanzisha na kuendeleza kwake mizozo ya ndani kwa muda mrefu kumepunguza pakubwa uwezo wa jeshi katika kukabiliana na wanamgambo wa Palestina kama tulivyoshuhudia likishindwa kihistoria na wanamapambano wa Hamas kupitia operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.
Tunaweza kusema kwamba mawaziri wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri la Netanyahu, kama vile Itmar Ben Gvir, sio tu kwamba hawasikitishwi na kushindwa kihistoria huko kwa jeshi huko Ghaza, bali wanafurahia jambo hilo kwa sababu lengo lao la kudhoofisha jeshi limetimia na hivyo kuandaliwa uwanja wa kuimarisha makundi ya wanamgambo wa Kizayuni wanaowataka wao. Inaonekana kwamba watu hao wanaongoza kwa makusudi jeshi la utawala huo kuelekea kinamasi kikubwa katika mgogoro wa Ghaza.