Sababu za kuakhirishwa vita vya ardhini dhidi ya Gaza
Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipaswa kuanzisha vita vya ardhini dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza kuanzia juzi, Jumapili, lakini uamuzi huo umeahirishwa.
Ijumaa iliyopita, katika siku ya saba ya vita vya Gaza, utawala wa Kizayuni wa Israel ulitangaza kuwa, utawapa wakazi wa kaskazini mwa Gaza muda wa saa 24 kuondoka katika eneo hilo, na kisha utaanzisha vita vya ardhini.
Gazeti la New York Times juzi liliwanukuu maafisa 3 waandamizi wa Israel na kutangaza kuwa, operesheni za ardhini au za nchi kavu za Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza zimeakhirishwa.
Ukweli wa mambo ni kuwa, vita hivi havijafutwa bali vimeahirishwa. Hujuma na mashambulizi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika kipindi cha siku 9 zilizopita yalikuwa makubwa mno kiasi kwamba katika muda huo Wapalestina karibu elfu 3 wameuawa shahidi na zaidi ya watu elfu 10 wamejeruhiwa. Kwa msingi huo, sababu ya kuahirishwa vita hivyo vya nchi kavu sio kwamba vita hivyo vitapelekea vifo vya maelfu ya watu, la hasha, bali kuna sababu nyingine.
Gazeti la New York Times limedai kuwa, sababu ya kuahirishwa kwa vita vya ardhini ni hali mbaya ya hewa katika eneo hilo. Gazeti hilo limenukuu mamlaka za Kizayuni na kuandika kuwa, hali ya anga haikuwa nzuri kwa ndege zisizo na rubani na marubani wa ndege hizo ambao walitakiwa kuvisaidia na kuunga mkono vikosi vya nchi kavu.
Pamoja na hayo, hiyo haikuwa sababu kuu ya kuakhirishwa kwa vita vya ardhini. Moja ya sababu kuu ni uwepo wa idadi kubwa ya raia wa kigeni huko Gaza na kwamba Marekani inajaribu kuwatoa watu hawa kutoka Gaza kwa kufungua tena kivuko cha Rafah.
Sababu nyingine muhimu inayotajwa na weledi wa mambo ni matokeo ya vita vya ardhini kwa utawala wa Kizayuni. Kuanzisha vita vya ardhini kutakuwa na maana ya kuchukua wigo mpana vita, jambo ambalo utawala wa Kizayuni hauko tayari kwa sasa.
Kwa muktadha huo, hapana shaka kwamba uamuzi mbaya zaidi ambao utawala wa Kizayuni unaweza kuuchukua ni kuingia Gaza kwa njia ya ardhini na kujiingiza katika vita vya miezi kadhaa vitakavyokuwa na hasara, jambo ambalo kwa hakika liko nje ya uwezo wa udhibiti wa Israel kijiografia, kieneo na kistratijia wa ardhi ndogo ya Gaza, na ni jambo lisilo na shaka kwamba, hilo litaleta hatari na changamoto nyingi kwa maghasibu Wazayuni.
Fauka ya hayo, Hamas imechimba njia za chini kwa chini na kuweka mitego kote Gaza na imegeuza maeneo ya chini ya ardhi ya Gaza kuwa kambi kubwa ya kijeshi yenye vifaa vya kutosha ambayo haitaruhusu Tel Aviv kuiteka kwa siku chache au wiki kadhaa chache.
Kadhalika, iwapo utawala dhalimu wa Israel utaingia katika ukanda wa Gaza kwa kutumia ardhi yake na kujaribu kuikalia tena kwa mabavu Gaza, kutaibuka kambi mpya katika vita hivyo ikiwemo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa kuzingatia kizazi cha vijana kilichounda makundi mapya ya muqawama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kuna uwezekano wa kufanyika operesheni za muqawama na kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kutoa kipigo kipya kwa utawala vamizi wa Israel.
Katika vita vya siku 51 vya 2014 na pia katika vita vya siku 22 vya 2008, wanajeshi wa Israeli walijaribu kuingia Gaza kwa njia ya nchi kavu na baharini, lakini walinaswa katika mitego ya milipuko na njia za chini kwa chini na askari wengi wavamizi waliangamizwa.
Katika miaka iliyopita, kambi ya muqawama imeonyesha kuwa, imekuwa na kuimarika katika uga wa kubuni operesheni, silaha, zana na mbinu za kijeshi, na yote hayo yanahesabiwa kuwa tishio kubwa dhidi ya Tel Aviv.
Ukweli ni kuwa, vita vya ardhini vinaweza kuwa kinamasi kikubwa kwa utawala unaoikalia kwa mabavu Quds na yumkini ukachezea kipigo kikubwa kuliko hata kile cha siku ya kwanza katika operesheni ya kijasiri ya Kimbunga cha al-Aqswa.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana wajuzi wa mambo wanaona kuwa, Israel inapasa kufikiri mara mbili mbili na kuchanga vyema karata zake kabla ya kuingia katika vita vya ardhini huko Gaza, eneo ambalo ni ngome kuu ya muqawama na mapambano ya Palestina.