Usitishaji vita wa siku 4 Gaza; sababu na ishara zake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105114-usitishaji_vita_wa_siku_4_gaza_sababu_na_ishara_zake
Hatimaye baada ya siku 47, utawala wa Kizayuni na Hamas wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku nne.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2023 23:34 UTC
  • Usitishaji vita wa siku 4 Gaza; sababu na ishara zake

Hatimaye baada ya siku 47, utawala wa Kizayuni na Hamas wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku nne.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mateka 50 wa Kizayuni wataachiliwa huru mkabala wa wafungwa 150 wa Kipalestina. Pia utawala wa Kizayuni utaruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.

Usitishaji mapigano huo umefikiwa kwa upatanishi wa Qatar na makubaliano ya Marekani. Kwa hivyo, sababu ya kwanza ya kufikiwa usitisha mapigano imekuwa ni Marekani kuyakubali. Hapo awali Wamarekani walikuwa wakipinga usitishaji vita kwa hoja kuwa ni kwa maslahi ya Hamas.

Sababu nyingine iliyopelekea kufanikiwa makubaliano ya usitishaji mapigano kwa muda ni kushindwa utawala wa Kizayuni kufikia malengo yake ya kijeshi huko Gaza dhidi ya Hamas. Hasa kwa kuzingatia kuwa, baraza la mawaziri la Netanyahu halikuweza kuwapata mateka wake waliokuwa wanashikiliwa na Hamas. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Kizayuni umeshambulia kwa mabomu hata hospitali na shule za Gaza zikiwemo shule zilizo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa madai kuwa mateka wake walikuwa mafichoni chini ya ardhi za shule na hospitali hizo. Wiki iliyopita Wazayuni walifanya maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wakitaka kusimamishwa vita na kuachiliwa huru mateka kutokana na utawala wa Kizayuni kushindwa kuwaachia huru mateka katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya raia wa Palestina.

Nembo ya Hamas

Jambo jingine muhimu ni mashinikizo ya kimataifa dhidi ya ukatili wa utawala wa Kizayuni. Maandamano yamekuwa yakifanyika katika pembe zote za dunia kwa ajili ya kulaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza na ambayo yameongezeka kwa kasi. Aidha waandamanaji wamelaani uungaji mkono wa wazi wa Marekani kwa jinai za utawala wa Kizayuni. Katika hali hiyo, serikali ya Washington, ambayo inakabiliwa na mashinikizo makubwa ya ndani, imeshinikiza baraza la mawaziri la Netanyahu kukubali usitishaji huo wa mapigano.

Nukta muhimu ni kwamba usitishaji vita uliotangazwa huko Gaza unamaanisha kushindwa utawala huo kufikiwa malengo iliyokusudia katika ukanda huo. Baada ya siku 47 za mashambulizi ya kila upande dhidi ya watu wa Gaza, utawala huo ghasibu hatimaye umelazimika kusalimu amri bila ya kufanikiwa kuuangamiza muqawama wala kupata mateka yeyote wa Kizayuni. Kusimamisha mashambulizi dhidi ya Gaza na kuwaachilia wanawake na watoto 150 wa Kipalestina katika hatua hii kunamaanisha kusalimu amri utawala huo mbele ya matakwa ya Hamas. Utawala huo umeshindwa kuwakomboa mateka wake katika kipindi cha siku 47zilizopita na umekubali tu kusitisha mapigano ili kubadilishana na kuachiliwa huru mateka wake 50, ili angalau kupunguza mashinikizo ya waliowengi  ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Hii ni pamoja na kuwa mateka 200 wa Kizayuni bado wako mikononi mwa Hamas na katika siku zijazo mateka hao wanaweza kutumiwa na kundi hilo la mapambano kama  turufu.

Hali ya kusikitisha ya watoto wa Gaza

Ukweli ni kwamba kukubali usitishaji vita bila ya kufikia malengo ya kijeshi ni kushindwa kwingine kwa utawala wa Kizayuni, jambo ambalo hata waziri mmoja wa baraza la mawaziri amelazimika kulikiri. 'Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni huku akitangaza kutoridhishwa kwake na usitishaji vita amesema kuwa, tunashuhudia tena mgawanyiko. Serikali ya Israel kwa mara nyingine tena imefanya kosa kubwa sana. Makubaliano yoyote ya kubadilishana mateka ni maafa na ishara ya ujinga wa baraza la mawaziri la vita.'