Israel yaanza tena kumwaga damu za Wapalestina Gaza, makumi wauawa shahidi
Miripuko kadhaa na milio ya risasi imesikika kaskazini mwa Ukanda wa Gaza baada ya utawala haramu wa Israel kuanzisha tena hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu, baada ya muda wa usitishaji vita kumalizika mapema leo.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti habari za kujiri makabiliano makali baina ya vikosi vya utawala wa Kizayuni na wanamapambano wa makundi ya muqawama wa Palestina huko Gaza.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Gaza imetangaza kuwa, jeshi katili la Israel mapema leo limeanzisha operesheni ya nchi kavu kaskazini magharibi mwa Gaza. Aidha utawala huo pandikizi umefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya ukanda huo.
Hadi tunamaliza kuandaa habari hii, utawala huo ghasibu ulikuwa umeshaua shahidi Wapalestina karibu 21 katika wimbi hilo jipya la hujuma na mashambulizi yake dhidi ya Gaza.
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Gaza, Ashraf al-Qudra amesema: Kwa akali Wapalestina sita wameuawa shahidi katika hujuma za anga katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.

Aidha watoto wengine wawili wameuawa shahidi katika shambulio jingine la anga la Wazayuni lililolenga jiji la Gaza, hayo yamesemwa na Fadel Naim, daktari katika Hospitali ya Al-Ahli.
Habari zaidi zinasema kuwa, ndege za kivita za Israel zimeshambulia kwa mabomu Hospitali ya Nasser mjini Khan Younis, kusini mwa eneo la Ukanda wa Gaza.
Mapema leo, ving'ora vilisikika katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni karibu na Gaza, huku Tel Aviv ikidai kuwa imetungua roketi lililovurumishwa kutokea Gaza.
Ikumbukwe kuwa, Jumatano iliyopita, baada ya siku kadhaa za mazungumzo, utawala wa Kizayuni na muqawama wa Palestina walifikia makubaliano ya usitishaji vita kwa muda wa siku nne na kubadilishana mateka. Jumatatu jioni utawala wa Kizayuni na harakati ya Hamas kwa upatanishi wa Misri, Qatar na Marekani walikubaliana kurefusha usitishaji vita huo kwa siku mbili, usitishaji vita ambao ulimalizika siku ya Alkhamisi na kurefushwa tena kwa siku nyingine moja hadi leo Ijumaa saa moja asubuhi.

Wapalestina zaidi ya 15,000 wameuawa shahidi tangu Israel ilipoanza kufanya jinai zake kwa karibu siku 50 dhidi ya wananchi wa Gaza mnamo Oktoba 7. Aidha idadi ya Wazayuni waliouawa katika Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni takriban 1,500, ambapo zaidi ya 380 ni wanajeshi.