Muendelezo wa maonyo ya serikali ya Uturuki kwa Israel
(last modified Sat, 09 Dec 2023 02:23:14 GMT )
Dec 09, 2023 02:23 UTC
  • Muendelezo wa maonyo ya serikali ya Uturuki kwa Israel

Huku mzozo wa kiuchumi ukiendelea kushika kasi nchini Uturuki, harakati za shirika la ujasusi la utawala wa kibaguzi wa Israel (Mossad) dhidi ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Kiislamu zinaendelea kuongezeka.

Serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa mara nyingine tena imeuonya utawala wa Kizayuni kuhusu operesheni yoyote ya Mossad dhidi ya Hamas nchini humo. Ali Yerli Kaya, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki ameuonya utawala wa Kizayuni kuhusu madhara makubwa ya uwezekano wa kutekelezwa operesheni ya Mossad dhidi ya wanachama wa kundi la Hamas la Palestina nchini humo. Akirejelea onyo la awali la vyombo vya usalama vya Uturuki kuhusu mipango ya kijasusi ya Mossad, Yerli Kaya amesisitiza kwamba jambo hilo halikubaliki kabisa na kuwa litaugharimu pakubwa utawala wa kigaidi wa Israel iwapo litatekelezwa.

Harakati mpya za kijasusi za utawala wa Kizayuni katika mataifa ya Kiislamu zinaashiria kuwa utawala huo wa kibaguzi kwa msaada wa majasusi wake wa ndani na nje, unajaribu kulazimisha matakwa yake dhidi ya mataifa hayo kwa kuwafuta kigaidi wapinzani wake wa kisiasa, hasa wanachama wa Hamas. Hivi karibuni, ripoti zimechapishwa kuhusu mpango wa shirika la ujasusi la Israel (Mossad) wa kutekeleza operesheni dhidi ya wanachama wa Hamas wanaoishi nje ya Palestina, wakiwemo wale wanaoishi katika nchi za Uturuki na Qatar. Ripoti hizo zimechapishwa kufuatia onyo la Uturuki kwa Wazayuni.

Ali Yerli Kaya, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki

Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa serikali ya Recep Tayyip Erdogan kuzungumzia hatua za kijasusi za Israel katika ardhi ya nchi hiyo. Kabla ya hapo, maafisa wa serikali ya Uturuki walikuwa wamezungumzia mara kadhaa kuhusu hatari ya ushirikiano wa masuala ya usalama na ujasusi kati ya Uturuki na utawala huo haramu. Maonyo ya mfululizo ya maafisa wa serikali ya Erdogan kwa Israel yanatokana na wasiwasi wao kuhusiana na harakati za kijasusi za Israel katika ardhi ya nchi hiyo.

Ni dhahiri kuwa, siasa za mauaji ya kigaidi dhidi ya wapinzani wa kisiasa wa Tel Aviv wanaoishi katika nchi tofauti za dunia ni moja ya sera rasmi za utawala ghasibu wa Israel. Tafiti na chunguzi zinathibitisha ukweli kwamba katika miongo kadhaa iliyopita, maelfu ya wapinzani wa kisiasa na kijeshi wa utawala huo wa Kizayuni wametekwa nyara na kuuawa kwa njia hiyo hiyo katika nchi mbalimbali. Kwa mfano, katika majira ya joto ya mwaka uliopita, kanali ya Al Jazeera ya nchini Qatar, ilionyesha filamu ya matukio ya kweli kuhusu shughuli za shirika la ujasusi la Israel, Mossad, nchini Uturuki, ambapo ilifichua habari za kutisha kuhusu shughuli zinazofanywa na majasusi wa shirika hilo dhidi ya viongozi wa mrengo wa mapambano ya ukombozi wa Palestina huko Uturuki.

Murad Aslan, mchambuzi na afisa wa zamani katika shirika la upelelezi la Uturuki, anasema:

"Utawala wa Israel hutumia mifumo, mbinu mbalimbali, mamluki na vibaraka wengi kupata na kupokea taarifa zozote unazozifuatilia. Lakini kosa lolote linalofanywa na mmoja wa vibaraka hao huharibu matokeo yote ya shughuli hizo za ujasusi."

Mtaalamu na mchambuzi huyo wa masuala ya ujasusi wa Uturuki anaendelea kusema:

"Makosa yaliyofanywa na maafisa wa Mossad ndiyo yalipelekea kugunduliwa mtandao wa kuajiriwa makurutu wapya wa Mossad huko Istanbul, jambo ambalo lilipelekea maafisa usalama wa Uturuki kufuatilia mienendo ya mtandao wa majasusi wa Israel na kugundua mipango ya Mossad."

Kufuatia kuonyeshwa filamu ya shughuli za majasusi wa Israel nchini Uturuki katika Televisheni ya Al Jazeera, vyombo vya habari vya Uturuki pia Oktoba mwaka jana vilionyesha sehemu ya kukiri Seljuq Kuchuk Kaya, kibaraka mkuu wa mtandao wa ujasusi wa Israel nchini Uturuki ambaye alisema:

Shirika la ujasusi la Mossad

"Mojawapo ya majukumu niliyopewa na Mossad ilikuwa ni kuajiri askari jeshi waliotoroka jeshini au wale waliostaafu katika jeshi la Uturuki na kuwapa mafunzo ili kulinda nyaraka za siri."

Maungamo hayo yanadhihirisha ukweli kwamba utawala wa kibaguzi wa Israel hauna rafiki wala mshirika usiyeweza kumfanyia ujasusi na wala hauna lengo jingine isipokuwa kutoa pigo dhidi ya mataifa mengine ya dunia na hasa nchi za Kiislamu. Kuhusiana na hilo, Uturuki na Jamhuri ya Azerbaijan zikiwa nchi za Kiislamu zinazojiarifisha kuwa marafiki na washirika wakubwa wa utawala wa kibaguzi wa Israel, zinafahamu vizuri lengo hilo la utawala ghasibu wa Israel. Pamoja na hayo inasikitisha kuona kuwa, ukweli kwamba Israel inayalenga zaidi mataifa ya Kiislamu duniani kwa jinai zake, ni suala muhimu ambalo viongozi wengi wa nchi za Kiislamu hawalitilii maanani.