Wanamapambano Palestina: Tumejiandaa kukabiliana na hujuma tarajiwa za Israel
-
Wanamuqawama wa Palestina
Wanamapambano wa Kipalestina wametangaza azma yao kamili kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi tarajiwa ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza.
Wanamapambano wa vikosi vya Al-Quds tawi la kijeshi la Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina walitangaza jana Jumatatu kwamba, katika radiamali ya vitisho mtawalia vya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel juu ya kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, kama ilivyo kawaida wamejiandaa vilivyo dhidi ya utawala huo. Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo imeongeza kuwa, wanapambano wataendelea kusimama imara katika kulinda taifa la Palestina kutokana na vitisho vya utawala wa Kizayuni. Akiongea katika baraza la mawaziri la Israel, siku ya Jumapili iliyopita, Avigdor Lieberman, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Kizayuni alitishia kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza. Itakumbukwa kuwa, katika vita vya siku 50 dhidi ya eneo hilo hapo mwaka 2014, jeshi la utawala katili la Israel liliua zaidi ya Wapalestina 2300, huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa. Katika hatua nyingine, Ahmad al-Awri, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa arakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesisitizia umuhimu wa kuendelezwa Intifadha sanjari na kuhitimishwa tofauti baina ya makundi ya Palestina. al-Awri ameyasema hayo katika hafla ndogo mjini Ramallah, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amesema kuwa, Intifadha ya Quds, ni msingi wa kufikiwa matukufu ya Wapalestina na kwamba harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu inaiunga mkono intifadha hiyo.