Masharti ya Muqawama wa Wapalestina ya usitishaji vita huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107986-masharti_ya_muqawama_wa_wapalestina_ya_usitishaji_vita_huko_gaza
Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Ziyad al Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina wamefanya mazungumzo kuhusu mapendekezo ya kusimamishwa vita Gaza na kutoa masharti yao kuhusu jambo hilo.
(last modified 2024-02-04T04:14:15+00:00 )
Feb 04, 2024 04:14 UTC
  • Masharti ya Muqawama wa Wapalestina ya usitishaji vita huko Gaza

Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Ziyad al Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina wamefanya mazungumzo kuhusu mapendekezo ya kusimamishwa vita Gaza na kutoa masharti yao kuhusu jambo hilo.

Katika mazungumzo yao hayo, harakati mbili za HAMAS na Jihadul Islami zimesema kuwa, mapendekezo yoyote ambayo hayatopelekea kusimamishwa kikamilifu uvamizi wa Israel huko Gaza, hayakubaliki kwa namna yoyote ile.

Pande hizo mbili zimesema, mazungumzo yoyote ambayo hayatopelekea kumalizwa vita na kuondoka wanajeshi vamizi wa Israel nje ya Ukanda Gaza pamoja na kuondolewa mzingiro na kujengwa upya ukanda huo hayawezi kukubaliwa na harakati hizo, na hakuna mabadilishano yoyote ya mateka maadamu masharti hayo hayajatimia.

Baada ya mazungumzo hayo harakati hizo mbili zimetoa taarifa ya pamoja na kusema kuwa, mazungumzo yoyote yale lazima yapelekee kukomeshwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, kuondoka wanajeshi wa Israel Ukanda wa Gaza, kuhitimishwa mzingiro wa eneo hilo pamoja na kujengwa upya maeneo yote yaliyoharibiwa kiuadui na Wazayuni maghasibu.

Wawakilishi wa utawala wa Kizayuni, Marekani, Misri na Qatar hapo awali walifikia makubaliano mjini Paris kuhusu fremu ya kusimamisha vita na kuwaachia huru wafungwa wengine wa jeshi la utawala huo ghasibu wa Israel na Hamas.

Hamas wakikabidhi mateka wa Israel katika moja ya mabadilishano ya mateka na utawala ghasibu wa Israel

 

Kulingana na mpango huo uliopendekezwa, usitishaji vita kamili na uondoaji kamili wa vikosi vya Israeli kutoka Gaza, kudhamini usalama kwa wakimbizi, kujenga upya Gaza na kuvunjwa mzingiro na kubadilishana wafungwa ni mambo ambayo yanapaswa kutekelezwa.

Tangu kuanza kwa operesheni ya tarehe 7 Oktoba na mafanikio ya dhahiri wazi ya vikosi vya muqawama, tarehe 24 Novemba 2023, takriban siku hamsini baada ya kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni ulilazimika kukubali masharti ya vikosi vya muqawama ya usitishaji mapigano kwa muda.

Viongozi wa utawala wa Kizayuni walitoa ahadi ya ushindi dhidi ya Hamas na kuidhibiti Gaza. Lakini baada ya muda kupita ilidhihirika kwamba uwezo wa vikosi vya muqawama ni mkubwa zaidi kuliko matarajio yao ya awali.

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lililazimika kuondoka katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Gaza katika marhala kadhaa baada ya kupata hasara kubwa na uharibifu mkubwa wa silaha za kijeshi, na pia kuondoka sehemu kubwa ya jeshi la Kizayuni katika maeneo yenye migogoro.

 

Kwa hakika matukio ya Gaza baada ya kimbunga cha Al-Aqsa ni kielelezo cha uwezo mpya na wa kustaajabisha wa vikosi vya mapambano ya Palestina. Vikosi vya upinzani vilifanikiwa kuwalazimisha wanajeshi wa Kizayuni kurudi nyuma katika mapigano mengi ya ana kwa ana. Utumiaji wa zana za hali ya juu za silaha pia ilikuwa sehemu muhimu ya uwezo wa makundi ya muqawama wa Palestina, jambo ambalo lililishangaza jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na viongozi wa utawala huo ghasibu na kuwalazimisha kukubali kushindwa.

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ehud Olmert alikiri kwamba Tel Aviv haina nguvu ya kuzuia harakati ya Hamas huko Gaza. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa utawala wa Kizayuni alimkosoa vikali Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri kwa kusema: Baraza la mawaziri la sasa la Israel limeinamisha kichwa mbele ya Harakati ya Hamas, na Wapalestina wametujengea  shule na kuifundisha somo Israel.

Katika siku za hivi karibuni, mamlaka na viongozi wa utawala wa Kizayuni wamekiri mara kwa mara juu ya kutokuwa na uwezo na kuwa katika hali mbaya mbele ya makundi ya muqawama wa Palestina katika hali ambayo, utawala huo kama ilivyo siku zote umekuwa ukinufaika na uungaji mkono wa kiuchumi na kijeshi wa Marekani na nchi za Magharibi.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki na tuhuma za mauaji ya halaiki ilikuwa kashfa nyingine kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wao katika Ikulu ya Marekani. Hata hivyo kwa kunyamaza kwao kimya, mamlaka za nchi za Magharibi hazijaonyesha jibu ipasavyo kuhusiana na tuhuma dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Wakati wa kukaribia kuingia mwezi wa tano tangu kutekelezwa operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa, makundi ya muqawama wa Palestina yanakamilisha mafanikio yao ya kijeshi kwa mafanikio ya kisiasa, na bila shakka kukubaliwa masharti yao makuu na ya kimsingi katika mazungumzo ya usitishaji vita ni ishara ya wazi ya udhaifu na kutokuwa na uwezo utawala wa Kizayuni wa Israel mbele ya makundi ya mapambano ya Palestina.