Baraza la Mawaziri la Israel linaelekea kusambaratika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i109494-baraza_la_mawaziri_la_israel_linaelekea_kusambaratika
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limefichua kwamba, duru za karibu na Baraza la Mawaziri la Israel zinasema kuwa, serikali hiyo inakariba kusambaratika kutokana na kushadidi hitilafu ndani ya baraza hilo.
(last modified 2024-03-14T08:41:50+00:00 )
Mar 14, 2024 08:41 UTC
  • Baraza la Mawaziri la Israel linaelekea kusambaratika

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limefichua kwamba, duru za karibu na Baraza la Mawaziri la Israel zinasema kuwa, serikali hiyo inakariba kusambaratika kutokana na kushadidi hitilafu ndani ya baraza hilo.

Duru za habari za Kizayuni zinaripoti kwamba, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel anafikiria jinsi ya kulivunja baraza la vita na kupeleka maamuzi yake kwa baraza kubwa la mawaziri.

Kwa upande mwingine, matokeo ya hivi punde ya uchunguzi yanaonesha kuwa, wakaazi wengi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu wanaamini kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa sasa na kiongozi wa Chama cha Likud, hataweza kushikilia nafasi ya Uwaziri Mkuu.

Kulingana na utafiti huu, umaarufu wa chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu umepungua na iwapo uchaguzi utafanyika, kitaweza kushinda viti 21 pekee.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Hivi karibuni, Yair Lapid, kiongozi wa chama cha upinzani cha Yesh Atid alikiri juu kushadidi hitilafu na mizozo ya ndani baina ya vyama vya upinzani na Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kauli hizo mpya za Lapid zinakuja wakati ambao mivutano ya kisiasa huko Tel-Aviv imefikia katika  kilele chake. Baraza la Mawaziri la Netanyahu kivitendo halijafanikiwa katika vita vya Gaza, na kushindwa mtawalia kwa jeshi la Kizayuni kumeiweka rehani nafasi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu pamoja na Baraza lake la Mawazri ambalosasa linaonekana kukalia kuti kavu.