Mar 17, 2024 10:57 UTC
  • Muqawama wa Iraq: Milango ya kuzimu itafunguka; watoa kauli ya mwisho kwa vikosi vamizi vya Marekani

Baada ya wiki moja ya kukaa kimya kimkakati, moja ya makundi ya harakati kubwa ya muqawama ndani ya kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq cha Hashdu al Shaabi limetangaza wazi msimamo wake kuhusu masuala muhimu ya usalama wa taifa. 

Kundi la Kata'ib Hizbullah (KH) limeikumbusha serikali ya Iraq na maafisa wa kamati iliyopewa jukumu la kusimamia mchakato wa kuondoka wanajeshi vamizi nchini Iraq kwamba hawapasi kutoa kinga kwa vikosi vamizi la sivyo milango ya kuzimu itafunguka kwa wanajeshi wote vamizi waliopo katika ardhi ya Iraq.

Kata'ib Hizbullah imeeleza haya ikiwalenga waziwazi wanajeshi vamizi zaidi ya 2,500 wa Marekani walioko katika kambi mbalimbali za kijeshi huko Iraq na maelfu ya wengine waliopiga kambi katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa matamshi haya ya Abu Ali al Askari Mkuu, Idara ya  Usalama ya harakati ya Kata'ib Hizbullah yameelekezwa kwa viongozi wa Iraq na ni onyo kwa Washington kwamba wakati umefika wa kufunga virago na kuondoka Iraq. 

Abu Ali al Askari 

Zaidi ya mwezi mmoja uliopita, makundi ya muqawama ya Iraq yalisitisha mashambulizi kwenye kambi za Marekani huko Iraq na Syria. Mashambulizi hayo yalikuwa yakifanywa na muqawama wa Iraq kuonyesha mshikamano na raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza na kwa lengo la kuwafukuza wanajeshi vamizi wa Marekani baada ya nchi yao kushiriki katika mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. 

Tags