Wapalestina wengine 60 wauawa na jeshi la Israel huko Gaza
(last modified Fri, 24 May 2024 03:00:40 GMT )
May 24, 2024 03:00 UTC
  • Wapalestina wengine 60 wauawa na jeshi la Israel huko Gaza

Makumi ya watu wakiwemo watoto wadogo na wanawake wanaripotiwa kuuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni ya al-Jazeera, watu zaidi ya 60 wameuawa shahidi katika mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza, hasa kusini mashariki mwa mji wa Rafah na katika eneo la Jabalia.

Kabla ya hapo, wanajeshi makatili wa Kizayuni waliwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 16 wakiwemo watoto watano na kuwajeruhi makumi ya wengine kwa kushambulia kwa mabomu msikiti na skuli katika kitongoji cha Ad-Darj katikati mwa mji wa Gaza.

Mashambulio hayo ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel yangali yanaendelea katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza katika hali ambayo, jamii ya kimataifa inaendelea kuishinikiza Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC itoe waranti wa kukamatwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel.

Jinai za Israel huko Gaza

Tangu ilipoanza operesehni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba, 2023, jeshi la utawala ghasibu wa Israel limeshaua shahidi watu 35,800 katika Ukanda wa Gaza na kuwajeruhi wengine zaidi ya 80,000.

Aidha kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadu (OCHA), asilimia 40 wa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.