IFRC yataka Israel isitishe mashambulizi katika Ukanda wa Gaza
Mtandao mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu duniani umesisitizia udharura wa kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza, eneo ambalo mamilioni ya Wapalestina wanakabiliwa na baa la njaa.
Jumuiya ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) imebainisha wasiwasi wake kutokana na mgogoro wa kibinadamu unaozidi kushtadi kila uchao katika Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Rais wa jumuiya hiyo, Kate Forbes ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Tunahitaji mno suluhu ya kisiasa itakayopelekea kufikiwa usitishaji vita na kutuwezesha kufikisha misaada ya kibinadamu (Gaza)."
Aidha Forbes ambaye Disemba iliyopita aliteuliwa kuwa mwanamke wa pili kuuongoza mtandao huo mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu duniani ametahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu katika mji wa Rafah na kusema kuwa, hali ya mambo katika eneo hilo la kusini mwa Ukanda wa Gaza inatisha.

Ameongeza kuwa, taasisi za kimataifa zinafanya kazi kwa mwendo wa kinyonga katika kushughulikia matatizo ya wakazi wa ukanda huo licha ya wakazi wa eneo hilo kukabiliwa na mauaji ya kimbari, kuhamishwa kwa nguvu na kubomolewa nyumba na miundombinu.
Mashambulizi ya wiki tatu ya Israeli dhidi ya mji wa Rafah yameibua hasira kote duniani hususan baada ya shambulio la anga la Jumapili (Mei 26) katika kambi ya wakimbizi lililosababisha Wapalestina wasiopungua watu 45.