Wanajeshi wa Iraq waikaribia ngome kuu ya Daesh, Mosul
Wanajeshi wa Iraq wamekaribia kufika kwenye mji wa Mosul ambao ni ngome kuu ya kundi la kigaidi la Daesh yaani ISIS, katika juhudi za Baghdad za kuwafurusha magaidi hao katika kona zote za nchi hiyo.
Shirika la habari la Sputnik limemnukuu Sabah al Numan, msemaji rasmi wa askari wa kupambana na ugaidi wa Iraq akisema kuwa, mji wa Mosul unakaribia kukombolewa, kwani askari wa nchi hiyo wameshafika umbali wa kilomita 60 kutoka katikati ya mji huo ambao ndiyo ngome kuu ya magaidi wa Daesh nchini Iraq.
Taasisi ya kupambana na ugaidi ya Iraq aidha imesema kuwa, vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kukomboa majengo ya makazi ya raia karibu na kituo cha jeshi la anga cha al Qayyarah, cha kusini mwa mji wa Mosul.
Magaidi 18 wa Daesh wameangamizwa katika operesheni ya kukomboa eneo hilo la makazi ya raia, na magari mawili yaliyokuwa yametegwa mabomu na magaidi, nayo yameharibiwa na jeshi la Iraq.
Wakati huo huo Haidar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iraq amewataka wananchi wa Mosul wajiandae kwa ajili ya ukombozi wa mji wao. Ametoa mwito huo baada ya jeshi la Iraq kukomboa kambi ya jeshi la anga ya Qayyarah, iliyoko umbali wa kilomita 60 kutoka mjini Mosul.