Jun 17, 2024 06:49 UTC
  • Haniya: Dalili za mgawanyiko zinaonekana wazi ndani ya utawala wa Kizayuni

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema ishara zote zinaonesha kuwa kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel, huku vita dhidi ya Wapalestina wasio na hatia vikiendelea katika Ukanda wa Gaza.

Ismail Haniyah alisema hayo jana Jumapili katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Adh'ha na kuongeza kuwa, "Adui ameshindwa kufikia malengo yake katika uvamizi, na hivi sasa dalili za migawanyiko zinaonekana katika safu za adui."

"Sikukuu ya Idul Adh'ha imekuja tena, lakini Ukanda wa Gaza unapambana na adui mvamizi kutoka kila upande," ameeleza bayana Ismali Haniya katika salamu zake hizo za Iddi.

Afisa huyo mwandamizi wa HAMAS amesisitiza kuwa, kundi hilo la muqawama katu halitasalimu amri, bali litaendeleza mapambano yake ya ukombozi kwa nguvu zote. Amesema jibu la HAMAS kwa mapendekezo ya usitishaji vita linaendana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS vile vile ameishukuru Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Harakati ya Ansarullah ya Yemen kwa uungaji mkono katika mapambano dhidi ya adui Mzayuni.

Wapalestina 40,000 walishiriki Swala ya Idul Adh'ha Masjdul Aqsa Jumapili Juni 16

Makumi ya maelfu ya Wapalestina jana Jumapili walishiriki katika Swala ya Iddul Adh'ha kwenye Msikiti wa al-Aqsa mjini Baitul Muqaddas, licha ya kuwekewa vizuizi na kukabiliwa na hatua kali za kiusalama zilizochukuliwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika mji huo unaoukalia kwa mabavu.

Aidha Swala ya Iddi iliswaliwa katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS mjini al-Khalil, huku maelfu ya Wapalestina wengine wakitekeleza ibada hiyo kando kando ya vifusi vya Misikiti na majengo yaliyobomolewa na mabomu ya Wazayuni.

Tags