Jun 20, 2024 02:56 UTC
  • Israel yaongeza maambukizi ya homa ya ini kwa wakimbizi wa Ghaza

Duru za hospitali katika Ukanda wa Ghaza zimeonya kuhusu kuenea ugonjwa wa homa ya ini na jinsi utawala wa Kizayuni wa Israel unavyoeneza ugonjwa huo kati ya wakimbizi wa Palestina.

Saleh al-Hams, Mkuu wa Idara ya Wauguzi ya Hospitali ya Ghaza ametangaza kuwa, Wazayuni wavamizi wameweka vikwazo vikali vya kuingizwa mafuta ndani ya Ukanda wa Ghaza kama ambavyo wanazuia kikamilifu kuingizwa vifaa vya matibabu katika ukanda huo.

Msemaji huyo wa Wizara ya Afya ya Ghaza ameongeza kuwa, mashirika ya kimataifa yanapaswa kuchukua hatua haraka za kupeleka mafuta yanayohitajiwa na hospitali.

Wakati huo huo Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, wanajeshi makatili wa Kizayuni wameendelea kukanyaga sheria za kimsingi za vita katika Ukanda wa Ghaza. Ofisi hiyo yenye uhusiano na Umoja wa Mataifa imegusia jinsi Israel inavyotumia silaha zilizopigwa marufukuu dhidi ya raia na kutangaza kuwa utawala wa Kizayuni hautofautishi baina ya askari na raia na unafanya maangamizi makubwa ya umati huko Ghaza. 

Amezungumzia pia hali mbaya ya Ukanda wa Ghaza, na kusisitiza kuwa, hivi karibuni watu 27,000 katika ukanda huo wameambukizwa homa ya ini kutokana na kunywa maji na vyakula vichafu. Utawala unaokalia kwa mabavu unaharibu kwa makusudi mfumo wa afya katika Ukanda wa Ghaza na kuvuruga huduma za matibabu kwa kushambulia hospitali kwa makusudi.

Katika kipindi cha miezi 8 iliyopita ya mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kuzuia kuingia chakula, maji, dawa na mafuta katika eneo hilo lililozingirwa kila upande, limeiweka Ghaza kwenye ukingo wa baa la njaa na maradhi ya kila namna.