Jul 16, 2016 06:48 UTC
  • Hizbullah, Hamas zalaani shambulizi la kigaidi Nice

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) zimelaani shambulizi la kigaidi lililofanyika katika mji wa Nice nchini Ufaransa.

Tarifa iliyotolewa jana na Hizbullah imelaani vikali jinai hiyo ya kigaidi nchini Ufaransa na kusema ni sehemu ya ugaidi ulioenea katika dunia ya sasa ambao unalenga kuangamiza kizazi cha mwanadamu.

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika katika nchi za Magharibi ni mwangwi wa ugaidi ulioligubika eneo la magharibi mwa Asia na kuwasulubu watu wa eneo hilo.

Hizbullah imesema, magaidi wanatekeleza mipango ya baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu kwa kuua watu wasio na hatia na kutangaza kuwa, mashambulizi hayo yanawakumbusha tena wanadamu udharura wa kupambana na kung'oa mizizi ya ugaidi.

Vilevile Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea katika mji wa Nice huko Ufaransa na kutangaza kuwa, misingi ya kimaadili na kibinadamu ya harakati hiyo inapinga aina zote za misimamo mikali na ugaidi.

Shambulizi lililofanyika Alkhamisi usiku katika mji wa Nice huko Ufaransa limeua watu 84 na kujeruhi wengine 130, makumi miongoni mwao wanaripotiwa kuwa mahututi.

Tags