Ansarullah: Operesheni za majini za Yemen zimewatia hofu maadui
-
Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema nguvu kubwa ya jeshi la nchi hiyo imewatia hofu maadui.
Akizungumzia namna jeshi la nchi hiyo linavyokabiliana na wavamizi wa Marekani, Uingereza na Wazayuni, Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi, kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, amesema uwezo mkubwa wa kijeshi, makombora na mbinu za vita vya majini za nchi hiyo katika kukabiliana na "pande tatu za shari" vimewatia hofu maadui.
Al-Houth ameongeza kwa kusema kwamba, kabla ya kuanza operesheni ya jeshi la Yemen kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, Wamarekani walidhani kwamba wangeweza kulisimamisha jeshi la Yemen, lakini nguvu za kijeshi za Marekani hazikuweza kuzima operesheni hizo za jeshi la Yemen za kushambulia meli za utawala wa Kizayuni au zinazoelekea Israel.
Kiongozi wa Ansarullah pia amezungumzia taathira za operesheni za jeshi la Yemen dhidi ya meli za utawala katili wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na kusema, safari za meli za Israel zimepungua na kufikia karibu nusu na zimetatizika, na meli za utawala huo hazionekani tena katika naji ya Bahari Nyekundu.
Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuendelea kushambulia meli za utawala katili wa Israel hadi utawala huo utakaposimamisha mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza.