Mtego wa Marekani kwa Saudi Arabia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i113854-mtego_wa_marekani_kwa_saudi_arabia_nchini_yemen
Seyyid Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, amesema katika hotuba kwamba Marekani inajaribu kuisukuma tena Saudi Arabia katika vita vya pande zote na Yemen.
(last modified 2024-07-09T02:30:40+00:00 )
Jul 09, 2024 02:30 UTC
  • Mtego wa Marekani kwa Saudi Arabia nchini Yemen

Seyyid Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, amesema katika hotuba kwamba Marekani inajaribu kuisukuma tena Saudi Arabia katika vita vya pande zote na Yemen.

Vita vya Saudia dhidi ya Yemen vilisimamishwa vikiwa vimeingia katika mwaka wake wa tisa, lakini mwisho wake haukutangazwa rasmi. Mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Yemen yangali yanaendelea katika nyanja tofauti, lakini pamoja na hayo si tu kwamba pande husika hazijafikia muafaka, bali pia mzozo kati ya pande hizo umeongezeka. Pamoja na hayo, Saudi Arabia na Yemen zinasitasita kuanzisha vita vipya. Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen anaamini kuwa Wamarekani wanataka kuiingiza Saudi Arabia katika vita vya pande zote na nchi hiyo na kurejesha hali ya mvutano iliyokuwepo katika eneo katika miaka ya nyuma.

Kuna sababu kadhaa muhimu kuhusiana na suala hilo. Kwanza kabisa ni kuwa Wayemen walitoa pigo kubwa kwa Marekani katika vita hivyo. Baada ya Yemen kuanzisha mashambulizi dhidi ya meli za nchi za Magharibi zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni (Israel), kwa lengo la kuwaunga mkono watu wa Ukanda wa Gaza ambao wanauawa kwa umati na utawala wa Tel Aviv, Marekani na nchi nyingine kadhaa ziliunda muungano wa kijeshi wa wanamaji dhidi ya Yemen ambapo zimekuwa zikifanya mashambulizi ya kijeshi ya mara kwa mara dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Pamoja na hayo na kutokana na mapambano makali ya watu wa Yemen na  vile vile kutoshirikiana aghalabu ya nchi za dunia hususan nchi za eneo na muungano huo, mashambulizi hayo ya maadui hayajawadhoofisha Wayemen. Kuhusiana na hilo, Abdul Malik al-Houthi amesema kuwa nchi nyingi duniani hazikushirikiana na muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi na kuamua kuratibu safari za meli zao na serikali ya Sanaa.

Yemen yakabiliana na meli za Wamagharibi kutetea watu wa Ukanda wa Gaza

Moja ya mapungufu makubwa ya Marekani ni kwamba ilizisukuma nchi zilizoko kando kando ya Bahari Nyekundu kuunga mkono adui wa Israel dhidi ya watu wa Palestina, lakini haikuweza kuzishawishi nchi za Kiarabu na jirani na Yemen ziruhusu ardhi zao zitumike kwa ajili ya kushambuliwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Sababu ya pili ni kuwa Marekani inaamini kuwa Ansarullah ya Yemen inazidi kuimarika na kuwa mhusika mkuu na muhimu katika mhimili wa muqawama katika eneo. Hivyo njama ya Marekani kuzuia hali hii ni kuihusisha tena kijeshi Saudi Arabia nchini Yemen. Kwa maneno mengine ni kuwa, kupitia vita vipya vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, Washington inajaribu kuzuia kupata nguvu Wayemen na mhimili wa muqawama nchini humo.

Iwapo Saudi Arabia itanaswa katika mtego huo hatari wa Marekani na kwa mara nyingine kuanza vita vipya dhidi ya Yemen, suala hilo litakuwa na madhara nakubwa kwa Riyadh, jambo ambalo tayari Al-Houthi ametoa tahadhari ya kutosha kuhusiana nalo. Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen amesema hatutakaa kimya mbele ya hatua zao za kichaa za kutaka kuwaweka njaa watu wa Yemen na kuvuruga uchumi wao. Amesisistiza kuwa kushughulishwa Wayemen katika vita vya moja kwa moja kwa ajili ya kuwatetea watu wa Gaza hakuna maana kwamba hawawezi kukabiliana na hatua za kijinga za maadui. Amesema: "Saudi Arabia inapaswa kutambua kwamba hatutakaa kimya mbele ya vitendo visivyo vya busara na bila shaka tutalipiza kisasi; Benki dhidi ya benki, uwanja wa ndege wa Riyadh dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana'a na bandari dhidi ya bandari."

Nukta ya mwisho ni kwamba kuwa macho Saudia kunaweza kuvunja njama mpya ya Marekani dhidi ya Wayemen na kuruhusu utekelezwaji wa mipango ya maendeleo ya Muhammad bin Salman. La sivyo, kuanzishwa vita vipya na kunasa Saudia katika mtego wa Marekani kunaweza kuusababishia matatizo makubwa utekelezaji wa mipango hiyo.