Lapid: Netanyahu amepoteza udhibiti wa serikali, vita haviwezi kuendelea milele
-
Yair Lapid
Kiongozi wa upinzani wa Israel, There Is a Future, amesema leo Jumanne kwamba Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, amepoteza udhibiti wa vita, uhusiano wa kigeni na wa serikali yake, kwa sababu kila mtu ndani ya serikali yake anafanya anachopenda.
Gazeti la Israel la Maariv limemnukuu Yair Lapid akisema kuwa vita (dhidi ya Gaza) haviwezi kuendelea milele. Ameongeza kuwa Israel inataka vita vya muda mfupi na kwamba huwezi kuajiri askari wa ziada milele, akionya kuwa uchumi wa Israel hauwezi kustahimili suala hilo.
Kuhusu mpango wa kubadilishana mateka wa vita, kiongozi huyo wa chama cha "There Is a Future" ameeleza kwamba harakati ya Hamas imechukua hatua za kufanikisha mpango huo wa kuwarejesha watu waliotekwa nyara.
Lapid amesema kuwa taarifa iliyotolewa hivi majuzi ya ofisi ya Netanyahu ilikuwa na madhara na haikuwa ya lazima na ilivunja nyoyo za familia za wale waliotekwa nyara na wanamapambano wa Hamas.
Hivi majuzi, Lapid alisema kuwa anafanya kazi na viongozi wa upinzani kuiangusha serikali ya mrengo wa kulia ya Benjamin Netanyahu.