Abbas: Mauaji ya Haniyah yanalenga kurefusha vita vya Gaza
-
Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amesema Israel ilimuua kigaidi Mkuu wa Ofisi ya Ksiasa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniyah ili kuendeleza na kurefusha vita vyake dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
"Hakuna shaka kwamba madhumuni ya mauaji ya Haniyah ni kurefusha vita na kupanua wigo wake," Abbas aliliambia shirika la habari la serikali la Russia RIA katika mahojiano yaliyochapishwa jana Jumanne.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amebainisha kuwa, mauaji hayo ya Haniyah yatakuwa na athari hasi katika mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha vita na kuwaondoa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza.
Abbas pia ametoa wito kwa Israel kuacha "vitendo vyake vya uchokozi" dhidi ya watu wa Palestina na kuzingatia sheria za kimataifa na kutekeleza Mpango wa Amani wa Nchi za Kiarabu.
Mpango huo unaipa Israeli fursa ya kuwa na uhusiano wa kawaida na majirani zake wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) mkabala wa kukobolewa maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) aliuawa hapa mjini Tehran tarehe 31 Julai, siku moja baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.