Holocaust ya kweli inafanyika katika Ukanda Gaza
Ikiwa mtu anatafuta mfano halisi wa mauaji ya Holocaust, basi anapaswa kuupata huko Gaza, kwani utawala wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mbali na kuua moja kwa moja ya raia zaidi ya 40,000, pia umewaweka katika hatari ya kifo manusura wengine wa vita kuua kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kutumia mashinikizo mbalimbali.
Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza katika taarifa yake kwamba, tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu madhulumu wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023 wakaazi 40,405 wa Gaza wameuawa shahidi na wengine 93,468 wamejeruhiwa. Mbali na kuenea kwa uharibifu na njaa iliyoua mamia ya watoto wa Kipalestina na kuhesabiwa kuwa miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani, zaidi ya Wapalestina 10,000 pia wametoweka.
Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likielezea kusikitishwa kwake na kupunguzwa kwa operesheni za utoaji misaada huko Gaza, limeonya kuwa Wapalestina milioni mbili wa Ukanda wa Gaza, ambao wamekabiliwa na vita haribifu vya utawala ghasibu wa Israel, wanataabika kwa uhaba mkubwa wa chakula.
Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, watoto 14,750 wa Kipalestina wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka mitano katika Ukanda wa Gaza wanataabika kwa utapiamlo mkubwa.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limetangaza kuwa, tangu katikati ya Januari mwaka huu hadi sasa, karibu watoto 240,000 wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka mitano wametambuliwa kuwa na dalili za utapiamlo huko Gaza.
Licha ya indhari za mashirika ya kibinadamu na ya utoaji misaada pamoja na matakwa ya kimataifa ya kufunguliwa tena vivuko ili kuzuia njaa inayosababishwa na kukatishwa kwa misaada na kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa na majeruhi, lakini askari wa utawala ghasibu wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, tangu utekeleze shambulio dhidi ya mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza na kudhibiti ardhi ya Rafah na kivuko cha Karam Abu Salem bado umeendelea kufunga vivuko vya eneo hilo.
Katika muendelezo wa jinai zao katika Ukanda wa Ghaza, askari wa utawala wa Kizayuni wameendelea kukalia kwa mabavu na kufunga vivuko vya ukanda huo kwa muda wa siku 112 mtawalia. Umoja wa Mataifa unaonya kuwa, zaidi ya Wapalestina milioni mbili wa Ukanda wa Gaza, wameelekea katika maeneo ambayo yanadaiwa kuwa ya kibinadamu yaliyoainishwa kwa amri ya jeshi la Utawala wa Kizayuni. Lakini hali ni kinyume na uhalisia kwani huko nako wamezingirwa katika eneo dogo kabisa kuliko hata kitongoji cha Manhattan cha jiji la New York.
Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa, kutokana na amri za kuhama zilizotolewa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo, asilimia 90 ya wakaazi wa ukanda huo wameyakimbia makazi yao mara kadhaa.
Kwa mujibu wa tangazo la Umoja wa Mataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa, vituo vingi vya maji vya Gaza vimeharibiwa au kubomolewa kabisa wakati wa vita vya miezi 10 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, na hivyo kuongeza masaibu mengine katika mateso ya watu wa Gaza. Hali hii imeongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa mbalimbali na hivyo kuhatarisha maisha yao.
Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu hivi sasa wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni unatumia vibaya maji kama silaha katika vita dhidi ya Gaza mbali na mizingiro mingine dhidi ya Gaza. Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa, zaidi ya visa milioni 1.7 vya magonjwa ya kuambukiza vimethibitishwa huko Gaza huku vita hivyo vikiwa vimeharibu kabisa miundombinu mbalimbali kama ya umeme na kukata hata huduma chache zilizokuwa zikitolewa na hivyo kupelekea vituo vya afya kufungwa kikamilifu. Hatua hiyo ya kinyama ni wasiwasi mwingine kwa watu milioni 2.4 wa Ukanda wa Gaza ambao tayari wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu na matokeo ya kuhama mara kwa mara sambamba na magonjwa ya kuambukiza.
Wizara ya Afya ya Gaza inasema kuwa, hivi sasa takriban watu 20,000 wagonjwa na majeruhi huko Gaza wanahitaji kusafiri nje ya nchi kwa matibabu, na kusisitiza kuwa hakuna hata mmoja wao aliyeweza kuondoka Ukanda wa Gaza tangu kukaliwa kwa mabavu vivuko na wanajeshi wa Israel na hivyo maelfu kati yao wanakabiliwa na hatari ya kifo
Uhaba wa dawa na suhula za tiba na kuweko idadi kubwa ya wagonjwa na majeruhi huko Gaza, sambamba na kuuawa shahidi na kutekwa nyara idadi kubwa ya wafanyakazi wa sekta ya tiba wa Wizara ya Afya huko Gaza, kumewafanya wafanyakazi waliobakia wa wizara hiyo kukabiliwa uchovu na mashinikizo maradufu.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, akiungwa mkono na Marekani, amewaweka watoto wa Gaza katika hali ya njaa, na idadi ya watu wanaokufa shahidi kwa sababu ya njaa inaongezeka siku baada ya siku. Inaenekana kuwa, kubomoa na kuteketeza hospitali, kuwatesa wakimbizi na kugeuza maisha ya wakazi wa Gaza kuwa jahanamu sio jambo muhimu si kwa chinjanja Netanyahu wala waungaji mkono wake ambao siku zote wamekuwa wakipiga ngoma ya kutetea haki za binadamu na hata kuyashinikiza matafa mengine kwa madai ya kukiuka haki za binadamu.