Netanyahu katika kinamasi cha mivutano na mizozo ya ndani
-
Benjamin Netanyahu
Hali ya wasiwasi na mgogoro wa ndani ya Tel Aviv vimezidi kupamba moto kutokana na ongezeko la maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) na kuongezeka hitilafu kati ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, na wapinzani wake.
Maandamano dhidi ya Netanyahu yameongezeka sana kuhusiana na kutojali na udhaifu wake katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na Hamas. Baadhi ya wapinzani wa baraza la mawaziri la Israel pia wanamtuhumu Waziri Mkuu wa utawala huo kuwa ameshindwa kusimamia vita vya Gaza. Familia za mateka wa vita wa Israel pia zilitangaza Jumapili iliyopita kwamba, Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, amewasahau mateka hao. Taarifa iliyotolewa na familia hizo imesema: "Tunaomba watu wote wafanye uasi wa kijamii ndani ya Israel, serikali itatetereka kuanzia kesho." Yair Lapid, kiongozi wa vyama vinavyopinga baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni pia aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter) kwamba: Netanyahu anajihusisha na udanganyifu na hila.
Maandamano ya mitaani dhidi ya baraza la mawaziri la Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yamezidi kupamba moto, lakini ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni imekanusha usitishaji vita huko Gaza kutokana na chanjo ya watoto katika eneo hilo.
Maandamano dhidi ya Netanyahu na kutokuwa na uwezo wa kufanya mazungumzo ya kusitisha vita na Hamas yanaendelea katika miji mbalimbali huku polisi wa Israel wakiwashambulia na kuwapiga waandamanaji wanaopinga vita vya Gaza. Walowezi wa Kizayuni pia wamefanya maandamano mjini Tel Aviv wakitaka kutiwa saini mara moja makubaliano ya kubadilishana wafungwa na mateka wa vita na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina huko Gaza.
Tangu kuanza Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, Benjamin Netanyahu na mawaziri wenye misimamo mikali katika baraza lake la mawaziri wamekuwa wakizidisha vita na machafuko kwa ahadi ya kuiangamiza harakati ya Hamas na kuyafurusha makundi ya mapambano ya Palestina katika eneo la Gaza. Hata hivyo baada ya kupita karibu mwaka mmoja sasa wa vita hivyo, Hamas na makundi ya wapiganaji wa Palestina yamethibitisha kwamba, yana uwezo kamili wa kukabiliana na Wazayuni.
Vita vya Gaza vinaendelea kwa msaada wa kijeshi na kifedha wa Marekani na nchi za Ulaya lakini misaada hiyo haijaweza kupunguza migogoro ya ndani ya Israel, na hali ya Wazayuni inaendelea kuwa mbaya zaidi kuliko hapo awali.
Makundi ya Muqawama ya Palestina yanasisitiza matakwa yao halali katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na utawala wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa wakimbizi wa Kipalestina katika maeneo yao na kuondoka kikamilifu askari vamizi wa Israel huko Gaza.
Alaa kulli hal, matokeo ya sera za vita za Netanyahu ni kutoweka imani ya vyama vya upinzani katika bunge la Kizayuni, na sasa wapinzani wanapanga kuitisha uchaguzi wa mapema.
Hapana shaka kwamba, katika hali hiyo, migogoro ya ndani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Isarel) itazidi kupamba moto kutokana na kuendelea vita vya Gaza, na Netanyahu atalipa gharama kubwa ya sera zake za kuchochea machafuko na mivutano yake na makundi yenye misimamo mikali ndani ya utawala huo ghasibu.