HAMAS yaangamiza na kujeruhi wanajeshi wengine wa Israel katika mtego kabambe
Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeonesha namna iliyoweka mtego kabambe katika mji wa Jenin kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuangamiza na kujeruhi wanajeshi kadhaa wa utawala wa Kizayuni.
Katika taarifa yake ya kijeshi, HAMAS imesema kuwa, wanamapambano wake leo wamewaingiza kwenye mtengo kabambe wanajeshi wa Israel na kuwazuia kusonga mbele na baadaye kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi hao magaidi wa Israel.
Taarifa hiyo ya HAMAS imeongeza kuwa, mara baada ya wanajeshi magaidi wa Israel kuingia kwenye mtego huo wamepokewa kwa mripuko wa bomu na mashambulizi ya risasi na kuangamizwa baadhi ya wanajeshi hao wa utawala wa Kizayuni na kujeruhiwa wengine.
Vile vile tawi hilo la kijeshi la HAMAS limesema kuwa lina mkanda wa video unaoonesha halikopta ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni ikitua kwenye eneo hilo kuzoa maiti na majeruhiwa hao.
Mapigano mengine yalitokea jana Jumapili jioni baina ya makundi ya muqawama ya Palestina na wanajeshi magaidi wa Israel katika mji wa Jenin kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina.
Jana asubuhi pia wanajeshi makatili wa Israel waliharibu eneo la biashara la mji wa Jenin na kuvunjia milango ya nyumba, kuvamia maduka na kufanya uharibifu mwingine mkubwa katika maeneo ya raia ikiwa ni kuzidi kuonesha ugaidi na ukatili wao mkubwa mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.