Takwa la Al-Azhar la kususiwa bidhaa za utawala wa Kizayuni
Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha Misri kimelaani jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na kutoa wito kwa Waislamu kususia bidhaa zinazotengenezwa na utawala wa Kizayuni.
Miezi 11 imepita tangu utawala ghasibu wa Israel uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza. Karibu Wapalestina 50,000 wameuawa shahidi na zaidi ya elfu 95 wamejeruhiwa katika uhalifu na jinai ambazo hazijawahi kutokea. Aidha hospitali na vituo vya matibabu, vyuo vikuu na shule, kambi za wakimbizi na nyumba zimebomolewa na kuharibiwa katika hujuma hiyo ya Wazayuni. Hata wagonjwa na watu waliokimbia makazi yao hawajasalimika na jinai za Wazayuni. Hakuna chakula wala dawa, huku njaa na magonjwa pia pamoja na mabomu vikitumiwa na Waazayuni kwa ajili ya kuwaua Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Hata hivyo, madola yenye nguvu duniani ama yanawaunga mkono Wazayuni katika jinai hii au yanatazama tu jinai hizo. Radiamali ya nchi za Kiislamu sio tofauti sana na mataifa yenye nguvu duniani. Kuonyesha wasiwasi wa maneno kuhusu jinai hizo kumewafanya Wazayuni waendeleze mauaji ya kimbari bila wasiwasi. Ukiacha makundi ya muqawama kama vile Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, Yemen ndiyo nchi pekee ya Kiarabu inayotoa msaada wa kioperesheni na kijeshi kwa watu wa Gaza.
Utawala wa Kizayuni ambao umeridhishwa na kuendelea mauaji ya halaiki na wala hauna wasiwasi na nchi za Kiarabu na madola yenye nguvu duniani, umeanza kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika duru yake mpya ya jinai.
Katika radiamali yake kwa mashambulizi hayo, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimetoa taarifa kikilaani mashambulizi hayo. Taarifa ya al-Azhar imesisitiza kuwa: Tunauomba ulimwengu wa Kiislamu uunge mkono kampeni ya kususia bidhaa zinazozalishwa na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuliunga mkono taifa la Palestina, msikiti wa Al-Aqswa na mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, na kujibu uchokozi dhidi ya ndugu zetu wa Kipalestina.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni kushambulia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hususan mji na kambi ya "Jenin" kwa siku kadhaa mtawalia ambapo mbali na kufanya uharibifu limewaua shahidi na kuwajeruhi makumi ya Wapalestina. Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Afya ya Palestina, makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza katika siku za hivi karibuni. Katika kipindi hiki, jeshi la Israel limewakamata makumi ya Wapalestina na kuharibu miundombinu na nyumba za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Takwa la Al-Azhar la kususiwa bidhaa zinazotengenezwa na Israel linaweza kuchukuliwa kuwa ombi la kimantiki na la kuridhisha, lakini wakati huo huo, inatarajiwa kwamba taasisi kama vile Al-Azhar nchini Misri ziitishe maandamano makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ili kulaani utawala wa Kizayuni na kulaani pia kutochukua hatua kwa tawala za Kiislamu katika kukabiliana na mauaji ya kimbari huko Gaza.
Bila shaka taasisi kama vile Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar cha Misri zinahesabiwa kuwa taasisi za marejeleo, na takwa lake la kususiwa bidhaa zinazotengenezwa na utawala haramu wa Israel na pia kufanya maandamano makubwa ya wananchi linaweza kuwa msingi wa mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni na mashinikizo dhidi ya tawala za Kiarabu ambazo zimenyamaza kimya na hata kwa kiasi fulani kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza zizinduke na kuacha kufanya hivyo.