Kuongezeka harakati za kundi la al-Qaeda nchini Afghanistan
Katika ripoti yake, jarida la Foreign Policy limedai kuwa, baada ya kundi la Taliban kutwaa tena udhibiti na madaraka nchini Afghanistan, nyayo na ishara za kundi la kigaidi la Al-Qaeda zinazidi kuonekana na kupanuka katika nchi hiyo. Jarida la Foreign Policy linasema, hilo linatokana na kuwa kundi la Taliban halifanyi juhudi kubwa kwa minajili ya kuyakandamiza makundi ya kigaidi, na hili linasababisha kupanuka wigo wa harakati za makundi kama al-Qaeda nchini Afghanistan.
Jarida hilo linasema katika ripoti yake hiyo kwamba, hadi kufikia sasa kundi la al-Qaeda limeanzisha zaidi ya kambi tisa mpya za kigaidi nchini Afghanistan. Ikiwa madai haya yatakuwa kweli, basi suala hilo linafanya majukumu ya kundi la wanamgambo wa Taliban wanaotawala nchini Afghanistan kuwa mazito zaidi.
Amin Farjad, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili:
Marekani inasema, katika fremu ya makubaliano ya Doha, Taliban imeahidi kutoruhusu kundi lolote la kigaidi kuendesha harakati zake nchini Afghanistan. Hata hivyo hilo halihusiani na yale makundi ambayo hayahatarishi usalama wa Marekani. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana harakati za makundi ya kigaidi nchini Afghanistan chini ya utawala wa Taliban haziwezi kuibua wasiwasi kwa Marekani.
Baadhi ya weledi wa mambo nchini Afghanistan wanaamini kuwa, Taliban imeruhusu kundi la kigaidi la al-Qaeda kuanzisha kituo na bohari za risasi katikati mwa Bonde la Panjshir. Kupuuza Taliban suala muhimu la kuimarisha usalama wa mipaka ya Afghanistan kumesababisha shughuli na harakati za makundi ya kigaidi kama vile al-Qaeda, tawi la Daesh la Khorasan na Tehreek-e-Taliban la Pakistan kuenea zaidi na zaidi nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa serikali ya Kabul, zaidi ya makundi 21 ya kigaidi yanayojulikana yalikuwa yakiendesha shughuli zake nchini Afghanistan kabla ya mwaka 2021, na inasemekana kuwa, shughuli za makundi hayo zimeongezeka na kuchukua wigo mpana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tangu wanamgambo wa Taliban washike tena hatamu za uongozi nchini humo..
Kwa mujibu wa Doug Livermore, afisa wa zamani wa Jeshi la Wanamaji na mjumbe wa Huduma Maalumu ya Operesheni ya Marekani ni kuwa, taa zote nyekundu zinamulika waziwazi na kuonya kuhusu harakati za makundi ya kigaidi nchini Afghanistan. Umoja wa Mataifa pia unaamini kwamba, kundi la kigaidi la Al-Qaeda kwa sasa limeanzisha kambi na vituo vya mafunzo katika angalau majimbo 10 kati ya 34 ya Afghanistan. Hii ina maana kwamba, kundi la kigaidi la Al-Qaeda linasajili wanajeshi kutoka nje ya Afghanistan na kuwapa mafunzo. Kwa sababu inasemekana kuwa, kundi la kigaidi la al-Qaeda limewataka wapiganaji wa kigeni kuhamia nchini Afghanistan na kujiandaa kwa ajili ya kushambulia maadui.
Ingawa hakuna habari za kuaminika kuhusu uwepo wa makundi ya kigaidi nchini Afghanistan, lakini ripoti zilizochapishwa kuhusu suala hili na duru za magharibi zinatia wasiwasi.
Upuuzaji wa Marekani katika suala hili, unaweza kuthibitisha maoni ya wachambuzi kwamba kwa kuondoka Afghanistan, Washington imo mbioni kuigeuza nchi hiyo kuwa mahali salama pa magaidi ili kwa njia hiyo ihatarishe usalama wa nchi za eneo likiwemo eneo la Asia ya Kati hadi katika mipaka ya China. Hapana shaka kuwa, Marekani ina taarifa za kina na za kutosha kuhusu harakati za makundi ya kigaidi nchini Afghanistan, lakini maadamu usalama wake na maslahi ya taifa hilo la kibeberu haviko hatarini, basi Washington daima itaendelea kuwasha taa ya kijani ambayo ni ishara ya kuruhusu na kutoa idhini ya kuendelea harakati hizo.