Wazayuni wenye misimamo mikali wavamia tena msikiti wa al-Aqswa
Mamia ya walowezi wa Kizayuni wamevamia tena msikiti mtakatifu wa wa Al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi dhidi ya kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Idara ya Wakfu za Kiislamu katika mji wa Baytul-Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu imetangaza kuwa, Jumatano ya jana zaidi ya walowezi 300 wa Kizayuni wenye misimamo mikali waliuvamia msikiti wa Al-Aqswa huku wakiungwa mkono na askari polisi wa utawala huo ghasibu.
Msikiti wa al-Aqswa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.
Walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali mara kwa mara wamekuwa wakivamia msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.
Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.