Saudia: Kuanzisha uhusiano na Israel kunategemea kutatuliwa kadhia ya Palestina
Sep 05, 2024 07:13 UTC
Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia amesema, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kunategemea kutatuliwa kadhia ya Palestina.
Bin Salman ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya hivi karibuni na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kuwa, hakutafikiwa mwafaka wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni pasi na kutatuliwa suala la Palestina.
Kabla ya hapo, Faisal Bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia naye pia alisema kwamba, serikali ya Marekani imeshaelezwa kuwa, bila kutambuliwa nchi huru ya Palestina kulingana na mipaka ya mwaka 1967, na Baitul Muqaddas Mashariki kuwa mji wake mkuu, sambamba na kukomeshwa mashambulio ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza na ukaliaji wa mabavu waeneo hilo hakuna uhusiano wowote wa kidiplomasia utakaoanzishwa na utawala wa Kizayuni.
Baada ya kupita miezi 11 tangu vilipoanzishwa vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza, mapigano makali yangali yanaendelea kati ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni na wapiganaji wa Muqawama katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, tangu vilipoanza vita dhidi ya ukanda huo Oktoba 7, 2023, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa kutokana na mashambulio ya kinyama ya Israel imeshapindukia elfu 40; na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya elfu 94, ambapo 33% kati yao ni watoto, 8.6% ni wazee na 18.4% ni wanawake.../