'Kaa' wa Israel waendelea kuwindwa kwa panga za Muqawama
Wanamapambano wa kambi ya Muqawama wameendelea kuwashinikiza Wazayuni ili wakomeshe jinai zao dhidi ya watu wa Ghaza kwa kutumia mbinu na njia mbalimbali na kwenye nyuga tofauti ikiwa ni pamoja na kukata mhimili wa kuusaidia utawala wa Kizayuni kwa njia za baharini.
Shirika la habari la FARS limeandaa ripoti maalumu na katika sehemu ya kwanza ya ripoti hiyo limemnukuu Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) akisema kuwa, Wazayuni walishambulia meli 14 za Iran katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Mediterania na sisi tukapiga meli 12 za Israel katika maeneo ya kaskazini mwa Bahari ya Hindi, tulipopiga meli ya tano tu, Wazayuni walinyanyua mikono juu ya kusema hawataki vita vya Meli.
Makala hiyo imeendelea kusema kuwa, vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni haviishii tu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na Israel kupata pigo kubwa la kiusalama, utawala wa Kizayuni ulikimbilia kwa madola ya kibeberu kuomba msaada na hadi hivi sasa unaendelea kupewa misaada ya kila namna na madola hayo hasa Marekani. Misaada hiyo ilitolewa kupitia angani na baharini.
Ripoti hiyo imeendelea kusema, kambi ya Muqawama haikukaa kimya bali inaendelea kutoa mashinikizo ya kila upande hususan kupitia kuzuia safari za baharini za vyombo vinavyopeleka misaada kwa utawala wa Kizayuni. Moja ya hatua hizo za kambi ya Muqawama ni kuvitwanga kwa silaha za kila namna vyombo hivyo vya baharini hasa katika Bahari Nyekundu na kuifunga kabisa njia hiyo ya baharini kutumiwa na vyombo vinavyoelekea katika ardhi za Palesitna zilizopachikwa jina bandia la Israel.
Ripoti hiyo pia imesema, ukitoa Yemen, kambi ya Muqawama imekuwa ikiishinikiza Israel ikomeshe jinai zake dhidi ya wananchi wa Ghaza kutokea nchi za Lebanon, Iraq na Syria na imeapa kwamba mapambano yataendelea hadi utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake huko Palestina.