Kupasishwa vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Bunge la Ireland
(last modified Sun, 10 Nov 2024 02:11:56 GMT )
Nov 10, 2024 02:11 UTC
  • Kupasishwa vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Bunge la Ireland

Wabunge wa Ireland wamepasisha muswada ambao unauarifisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni utawala mtenda jinai unaofanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza mbele ya macho ya walimwengu.

Kwa mujibu wa muswada huo, serikali ya Ireland imetakiwa kuuwekea utawala wa Kizayuni wa Israel vikwazo vya kibiashara, usafiri na kidiplomasia. 

Kwa kupasisha mpango huo, wabunge wa Ireland pia wameitaka serikali ya nchi hiyo kusimamisha mara moja miamala yote inayohusiana na zana za kijeshi na silaha na utawala wa Kizayuni, kuupiga marufuku utoaji wa leseni za usafirishaji wa bidhaa za matumizi pacha kwa utawala huo na pia kutangaza marufuku ya ndege zinazobeba silaha kuelekea Tel Aviv kutumia anga na viwanja vya ndege vya Ireland. 

Bunge la Ireland limepasisha mpango huu katika hali ambayo, Micheál Martin, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo pia aligusia uamuzi wa Dublin wa kuunga mkono kesi iliyowasilishwa na Afrika katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza. 

Hivi karibuni serikali ya Ireland ilitangaza kuwa, itaiwekea Israel vikwazo. Hatua hii ya Ireland imechukuliwa nje ya fremu ya Umoja wa Ulaya baada ya waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni ndani ya EU kufelisha jitihada za serikali ya Dublin na Uhispania katika uwanja huo. Nchi mbili hizi pamoja na Slovenia na Luxembourg zinaunda mrengo wa nchi zinazowaunga mkono watu wa Palestina barani Ulaya na zimejaribu kila ziwezalo kuzuia kuuzwa bidhaa za Israel barani Ulaya hasa bidhaa za vyakula na za viwanda. 

Harakati ya kususia bidhaa za Israel 

Umoja wa Ulaya ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Israel ambapo kiwango cha ubadilishaji wa kibiashara kati yake na utawala huo mwaka uliopita kilifikia karibu dola bilioni 50. Wakati huohuo, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Ireland, Uhispania na nchi nyingine kadhaa zilitaka kusitishwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel; na hilo liliungwa mkono na Josep Borrel, Kamishna wa Uhusiano wa Nje Umoja wa Ulaya. Hata hivyo nchi zinazouhami utawala wa Kizayuni, hususan Austria na Ujerumani, zilikwamisha utekelezaji wa hatua hiyo. Ireland na Uhispania kwa upande wao, zinasisitiza kuwa uamuzi huo ulipasa kutekelezwa kwa kuzingatia hukumu iliyotolewa na mahakama ya ICJ mwezi Julai mwaka huu kwamba uvamizi wa Israel kulikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Katika miezi kadhaa ya karibuni, kumetolewa ripoti kwamba Ireland inataka kuchukua hatua inayokinzana na Umoja wa Ulaya, yaani kuiwekea vikwazo Israel. Simon Harris Waziri Mkuu wa Ireland karibu wiki tatu zilizopita alitangaza kuwa nchi hiyo inafanya jitihada kuiwekea Israel vikwazo vya kiuchumi na inaamini kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kusaidia kutekelezwa uamuzi huo. Wataalamu wanasema kuwa kuna uwezekano Ireland ikaziwekea vikwazo bidhaa nyingine zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na Umoja wa Ulaya pia hautajibu na kutoa adhabu maalumu dhidi ya nchi hiyo kwa kuwa hautaki kusababisha mvutano wa ndani katika umoja huo.

Moja ya machaguo yaliyopo ni kupiga marufuku ununuzi wa bidhaa za chakula na nyingine zinazotengenezwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi hukko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Makadirio ya mahesabu yaliyofanywa huko Ireland yanaonyesha kuwa thamani ya bidhaa hizo inafikia yuro milioni moja kwa mwaka.  

Simon Harris, Waziri Mkuu wa Ireland

Tangu kuanza mashambulizi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza Oktoba 7 mwaka jana, uwanja wa harakati inayounga mkono kususiwa utawala huo imepitia mabadiliko makubwa. Baada ya kutekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, Oktoba 7 mwakak jana iliyofuatiwa na vita vya Gaza, baadhi ya malengo ya muda mrefu ya harakati ya kuisusia Israel na taasisi zinazoiunga mkono Palestina yamefikiwa. Hivi sasa jinamizi la viongozi wa Kizayuni katika uga wa kushadidi kutengwa utawala huo linazidi kuwa kubwa, ambapo vita vya Gaza vimeingia katika mwezi wa 14 sambamba na kuongezeka vikwazo dhidi ya Israel katika nyuga mbalimbali na hata katika nchi za Magharibi, zikiwemo za Ulaya na  huko Amerika ya Latini.