Wazayuni wafurahia jinai za magaidi nchini Syria
Maneno yanayosema: "Adui wa adui yetu anapigana na adui yetu" yamezidi kupata nguvu hivi sasa baada ya vyombo vya habari vya Kizayuni kushindwa kuficha furaha zao kutokana na jinai zinazofanya na magenge ya kigaidi nchini Syria. Huu ni ushahidi wa wazi kwamba matukio ya Syria yanatumikia moja kwa moja malengo ya kibeberu ya Wazayuni.
Faris al Sarfandi, mwandishi wa habari wa televisheni ya al Alam huko Ramallah amelinukuu gazeti la Kizayuni la Maarev likiandika: "Wanamapambano wa Erdogan wapambana na Kambi ya Muqawama..." na kusema kuwa, vichwa vya habari kama hivyo ndivyo vinavyoakisiwa sana hivi sasa na vyombo vya habari vya Kizayuni zikiwemo televisheni za Israel.
Naye Ashraf Akkah, mtaalamu wa masuala ya kiistratijia amemwambia mwandishi wa habari wa al Alam huko Ramallah kwamba, vyombo vya habari vya Kizayuni vinasherehekea matukio yanayoendelea Syria baada ya kuona magenge ya kigaidi na ukufurishaji yanafanya jinai nchini humo, ugaidi ambao unaonesha wazi kwamba umepata baraka zote za Israel na Marekani. Mtaalamu huyo amesema, cha kusikitisha zaidi ni kwamba vitendo vya magaidi hao vinalenga kukhafifisha mapambano ya kweli ya wanamapambano wa Palestina na Lebanon na jinsi utawala wa Kizayuni ulivyoshindwa kufikia malengo yake uliyoyatangaza huko Ghaza na Lebanon.
Kwa upande wake Ali Laour, mwandishi na mchambuzi wa kisiasa amemwambia mwandishi huyo wa habari wa televisheni ya al Alam kwamba furaha ya Wazayuni haionekani kwenye vyombo vya habari tu, bali imeenea pia kwenye ngazi za wanasiasa na maafisa usalama wa Israel, baada ya kuona magenge ya kigaidi yanafanya jinai dhidi ya wananchi wa Syria.