Jenerali wa Israel wa kusimamia faili la Iran atishia kujiuzulu
Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Israel ambaye anahudumu kama mkuu wa "Kurugenzi ya Mikakati ya Duara la Tatu," ambayo ina jukumu la kutunza mafaili ya masuala ya kijeshi ya Iran ndani ya utawala wa Kizayuni, ametangaza nia yake ya kujiuzulu.
Meja Jenerali Eliezer Toledano amewaambia wasaidizi wake kwamba hana mpango wa kugombea kuwa mkuu wa majeshi ya Israel na hatochukua tena jukumu lake la hivi sasa muda wake utakapoisha.
Haya yanajiri huku ripoti kadhaa za hivi karibu za vyombo vya habari zikimtaja Toledano kama mrithi wa mkuu wa majeshi wa Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi, ambaye alisema atajiuzulu baada ya uchunguzi wa jeshi kubaini kushindwa kugundua na kuzuia shambulio kubwa la kushtukiza lililoongozwa na Hamas na makundi mengine ya Muqawama ya Ghaza dhidi ya utawala wa Kizayuni, Oktoba 7, 2023.
Operesheni kabambe ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na HAMAS mwezi Oktoba 2023 imeufedhehesha vibaya utawala wa Kizayuni wa Israel na kovu hilo la aibu haliwezi kufutika hata siku moja. Kila leo maafisa mbalimbali wa Israel wanalazimika kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo.
Licha ya viongozi makatili wa Israel kufanya jinai kubwa dhidi ya Wapalestina ambapo taarifa zinasema kuwa, tokea Oktoba 7, 2023 ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari huko Ghaza hadi sasa, utawala wa Kizayuni umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 44,300 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi zaidi ya 105,000, lakini hauwezi kamwe kufidia fedheha uliyopata mwezi Oktoba 2023.