Syria yakomboa barabara kuu na maeneo muhimu, yaangamiza makumi ya magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119644-syria_yakomboa_barabara_kuu_na_maeneo_muhimu_yaangamiza_makumi_ya_magaidi
Jeshi la Syria limekomboa barabara kuu karibu na mji wa Hama pamoja na miji na vijiji vyote vinavyoizunguka barabara hiyo, na kuangamiza makumi ya magaidi wakufurishaji walioanzisha wimbi jipya la jinai katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2024-12-03T02:57:30+00:00 )
Dec 03, 2024 02:57 UTC
  • Syria yakomboa barabara kuu na maeneo muhimu, yaangamiza makumi ya magaidi

Jeshi la Syria limekomboa barabara kuu karibu na mji wa Hama pamoja na miji na vijiji vyote vinavyoizunguka barabara hiyo, na kuangamiza makumi ya magaidi wakufurishaji walioanzisha wimbi jipya la jinai katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Jana Jumatatu, vikosi vya Syria vilikomboa maeneo muhimu ikiwemo barabara kuu ya karibu na mji wa Hama ambayo inaunganisha miji ya Mahardeh na Suqaylabiyah na miji na vijiji vyake vyote vya karibu yakiwemo maeneo ya Karnaz, Tal Malah, al-Jalamah, Jabbin, Hayalin na Sheikh Hadid.

Hayo yamethibitishwa na vyombo mbalimbali vya habari ambavyo vimetangaza pia kuwa, takriban magaidi 80 zaidi, wakiwemo viongozi mashuhuri wa genge la ukufurishaji la Tahrir al-Sham au Jabhatun Nusra wameangamizwa katika operesheni za jeshi la Syria kwenye viunga vya Hama pamoja na maeneo ya mashambani ya Halab na Idlib ya kaskazini mwa Syria. 

Kabla ya hapo televisheni ya Syria ilikuwa imetangaza kuwa karibu magaidi 320 wameangamizwa katika miji hiyo mitatu wakati wa mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo ya Kiarabu na washirika wao wa Russia. Mashambulizi ya jana Jumatatu yameteketeza pia maghala 12 ya silaha za magaidi hao pamoja na kutunguliwa ndege moja isiyo na rubani ya magenge hayo ya kigaidi. 

Wakati huo huo duru za Russia zimeripoti kuwa, magaidi wa Jabhatun Nusra wanafanya njama za kupeleka gesi za sumu kwenye mikoa ya Halab na Idlib kwa ajili ya kuzitumia ili baadaye waituhumu serikali ya Damascus kama magaidi hao walivyozoea kufanya kwenye maeneo tofauti ya Syria mwaka 2014. Madai hayo ya uongo ya kutumiwa gesi za sumu yalitumiwa vibaya na Marekani, Uingereza na Ufaransa kama kisingizio cha kufanya mashambulizi makali na mabaya ya makombora mara kadhaa mwaka 2014 huko Syria.