Ugaidi wa kimataifa nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119654-ugaidi_wa_kimataifa_nchini_syria
Matukio ya siku za hivi karibuni nchini Syria kwa mara nyingine tena yameangazia suala la ugaidi wa kimataifa katika nchi hiyo.
(last modified 2024-12-03T04:08:02+00:00 )
Dec 03, 2024 04:08 UTC
  • Ugaidi wa kimataifa nchini Syria

Matukio ya siku za hivi karibuni nchini Syria kwa mara nyingine tena yameangazia suala la ugaidi wa kimataifa katika nchi hiyo.

Jumatano iliyopita, sambamba na kutangazwa kusitishwa mapigano kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel, ilitangazwa habari ya shambulio kali la kigaidi lililoongozwa na kundi la Tahrir al-Sham kaskazini mwa Syria; na tangu wakati huo mapigano makali na yaliyosambaa yangali yanaendelea kati ya jeshi la Syria na washirika wake dhidi ya magaidi wa kitakfiri.

Syria ilitumbukia katika vita na magaidi pia kuanzia 2011 hadi 2018. Machafuko ya hivi sasa nchini Syria yamejikita katika makundi ya kigaidi, lakini tofauti na kipindi cha miaka 7 iliyopita, safari hii hali ya magaidi hao ni tofauti.

Kwa upande mmoja, magaidi hawajagawanywa katika matawi mengi na karibu wote wanapigana chini ya bendera ya Tahrir al-Sham. Kwa upande mwingine, magaidi hao wana zana za kisasa zaidi, kama vile ndege zisizo na rubani za kujitoa mhanga, na hawaendeshi tu vita vya ardhini dhidi ya utawala wa Syria.

Suala jengine ni kuwa, tofauti na kipindi cha miaka 7 iliyopita, magaidi hao hawana mtazamo mkali kwa wananchi na wala hawakuleta hofu kubwa. Kwa upande wa vyombo vya habari pia, wanasimamia fikra kwa manufaa yao wenyewe, na huku wakichapisha habari za uongo kuhusu hali ya utawala wa Syria, kama vile mapinduzi dhidi ya Bashar Assad, pia wanaonyesha mafanikio yao katika uwanja huo.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

 

Mazingira hayo juu ya yote yanaashiria kuwa, harakati za magaidi zinasimamiwa na kupangwa na waungaji mkono wao wa kigeni hususan mhimili wa Kizayuni na Marekani na kwa mujibu wa balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, Syria inakabiliwa na ugaidi wa kimataifa.

Akigusia nafasi haribifu ya baadhi ya nchi za eneo katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi katika miji ya Hama na Idlib na kusababisha vita na umwagaji damu, Hossein Akbari balozi wa Iran nchini Syria amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia suhula zilizotolewa hivi karibuni kwa makundi hayo ya kigaidi, inaonekana makundi hayo yalikuwa na mawasiliano na nchi za Magharibi na za eneo kwa ajili ya kuchukua hatua kama vile kuajiri na kupanga vikosi, kuratibu na kutekeleza operesheni, ufuatiliaji na udhibiti, mwongozo na uongozi, mawasiliano na uratibu wa operesheni za kigaidi.

Kuwa pamoja vyombo vya habari vya Magharibi na magaidi hao katika uenezaji mkubwa wa habari za uwongo, habari bandia na video za upotoshaji zinazohusiana na matukio ya Syria ni sehemu ya vita vya kisaikolojia ambavyo nchi za Magharibi zimeanzisha kwa minajili ya kuunga mkono magaidi nchini Syria.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Syria ameesema: Kabla ya mashambulizi kuanza, maafisa kutoka Ulaya Mashariki walikuja Syria kuwafundisha magaidi jinsi ya kutumia ndege zisizo na rubani.

Baadhi ya weledi wa mambo wanaashiria historia ya Marekani ya kuwaunga mkono magaidi kuanzisha vita nchini Syria na eneo, na wanaashiria njama za hapo awali za Washington za kuunda makundi ya kigaidi kwa lengo la kuitenga Syria na kusema:

Magaidi wa Jabhat al-Nusra

 

Hapana shaka kuwa Marekani na washirika wake wanatekeleza njama ya kigaidi huko Syria. Weledi wa masuala ya kijeshi pia wanazungumzia nafasi na mchango wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuvuruga amani na usalama nchini Syria.

Mbali na ukanushaji na ukanaji wote unaotolewa na nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusiana na suala la kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria, lakini pazia la nchi hizo limeshafuniliwa kwa watu wa eneo hili kwa muda mrefu. Watu wa eneo la Magharibi mwa Asia daima wamekuwa wahanga wa mchezo mchafu wa nchi za Magharibi kwa madai ya kupambana na ugaidi katika miongo kadhaa iliyopita.