Gaza inaongoza kwa Watoto walemavu huku Israeli ikiendeleza mauaji ya kimbari
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119680-gaza_inaongoza_kwa_watoto_walemavu_huku_israeli_ikiendeleza_mauaji_ya_kimbari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema eneo la Gaza hivi sasa linaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliokatwa viungo vya mwili hasa mikono na miguu kutokana na vita vya Israel dhidi ya eneo hilo, na wengi wanapata upasuaji bila nusu kaputi.
(last modified 2024-12-03T23:59:19+00:00 )
Dec 03, 2024 23:59 UTC
  • Gaza inaongoza kwa Watoto walemavu huku Israeli ikiendeleza mauaji ya kimbari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema eneo la Gaza hivi sasa linaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliokatwa viungo vya mwili hasa mikono na miguu kutokana na vita vya Israel dhidi ya eneo hilo, na wengi wanapata upasuaji bila nusu kaputi.

Ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa mawaziri unaofanyika Cairo, Misri kwa lengo la kusaka suluhu ya la vita vya mauaji ya kimbari vya Gaza vilivyoanzishwa na utawala haramu wa Isarel Oktoba mwaka jana baada ya operesheni ya kulipiza kisasi ya harakati ya Hamas.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, Guterres amesema watoto hao waliokatwa viungo kwa mashambulizi wanapata tiba ya upasuaji bila nusu kaputi kwani mfumo wa afya Gaza umesambaratika na kwamba “kile tunachoona kinaendelea Gaza kinaweza kuwa uhalifu mkubwa wa kimataifa.”

Kabla ya vita vya sasa vya Gaza kuanza, karibu watoto 100,000 huko Gaza walikuwa na ulemavu. Vurugu za sasa zimesababisha maelfu zaidi kupata ulemavu wa kudumu, huku shirika la kimataifa la Save the Children likikadiria kuwa zaidi ya watoto kumi hupoteza angalau kiungo kimoja kila siku Gaza.

Mzingiro wa Isarel dhidi ya Gaza umezuia vifaa muhimu vya tiba kuingia eneo hilo, na kuwaacha watu wengi walemavu bila chakula, maji safi, au huduma ya matibabu. Ukosefu wa rasilimali umelazimisha familia kufanya maamuzi magumu, mara nyingi kutanguliza maisha ya kimsingi kuliko utunzaji maalum hasa wa walemavu.

Mashambulizi ya umwagaji damu ya utawala ghasibu wa Israel huko Gaza hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 44,466 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine zaidi ya 105,358. Maelfu zaidi pia hawapo na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.