Iran yasema wadhamini wa mazungumzo ya amani ya Syria watakutana Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119732-iran_yasema_wadhamini_wa_mazungumzo_ya_amani_ya_syria_watakutana_qatar
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ametangaza kuwa wanadiplomasia wakuu wa nchi tatu zilizodhamini mchakato wa amani wa Astana watakutana nchini Qatar kujadili kuzuka upya kwa ugaidi nchini Syria.
(last modified 2024-12-05T04:17:16+00:00 )
Dec 05, 2024 04:17 UTC
  • Iran yasema wadhamini wa mazungumzo ya amani ya Syria watakutana Qatar

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ametangaza kuwa wanadiplomasia wakuu wa nchi tatu zilizodhamini mchakato wa amani wa Astana watakutana nchini Qatar kujadili kuzuka upya kwa ugaidi nchini Syria.

Araghchi Jumatano alisema ataelekea Qatar "mapema wiki ijayo" ili kushiriki katika kikao cha Jukwaa la Doha.

Akibainisha kuwa wanadiplomasia wakuu wa Russia na Uturuki pia watakuwepo mjini Doha kushiriki katika mkutano huo, Araghchi alitangaza kuwa mkutano ujao wa mchakato wa Astana katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje utafanyika katika mji mkuu wa Qatar.

"Hakika, Qatar haitashiriki katika mkutano huu, na kwa kuwa mawaziri hawa wako Doha, tutafanya mkutano huko."

Iran na Russia, kama washirika wa serikali ya Syria, pamoja na Uturuki, ambayo ni upande wa upinzani, zilianzisha mchakato wa amani wa Astana mnamo Januari 2017, kwa nia ya kumaliza mzozo wa Syria, uliozuka mnamo 2011. Mchakato huo ulishirikisha serikali ya Damascus na upinzani.

Baada ya kuzuka tena kwa ugaidi nchini Syria wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekuwa mstari w mbele  kulinda mafanikio ya mazungumzo ya amani ya Astana.

Hayo yanajiri wakati magaidi wakiongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) wameanzisha mashambulizi makubwa nchini Syria Jumatano iliyopita, na kuteka maeneo yanayodhibitiwa na serikali kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Vikosi vya jeshi la Syria vinaendelea kupambana na magaidi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni katika eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, na kuwasababishia hasara kubwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, vikosi vya serikali ya Syria, vikisaidiwa na Russia na Iran, vimeweza kuchukua udhibiti wa karibu maeneo yote ya nchi hiyo..