AI: Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina
Kuna ushahidi "usio na shaka" kuwa Israel inafanya vitendo vya mauaji ya kimbari kwa "dhamira ya wazi ya kuwaangamiza Wapalestina."
Hayo yamesema na shirika la kimataifa kuteta haki za binadamu, Amnesty International katika ripoti iliyochapishwa leo Alhamisi. Shirika hilo limesema kwamba Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza.
Shirika hilo lenye makao yake mjini London Uingereza limesema limefikia natija hiyo baada ya miezi kadhaa ya kuchambua matukio na kauli za maafisa wa utawala wa Israel.
Uchunguzi wa Amnesty umebaini kuwa Israel imefanya vitendo vitatu kati ya vitano vilivyokatazwa chini ya mkataba wa mauaji ya kimbari ambayo ni mauaji, na kusababisha madhara makubwa ya mwili au kiakili na "kuwaweka kimakusudi Wapalestina katika Gaza hali ya maisha inayolenga kuwadhuru kimwili."
Utawala katili wa Israel ulianzisha vita dhidi ya Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 baada ya harakati ya muqawama wa Palestina Hamas kufanya operesheni ya ghafla ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu ili kulipiza kisasi jinai za miongo kadhaa za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Mashambulizi ya umwagaji damu ya utawala huo kwenye Gaza hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 44,532 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine zaidi ya 105,538. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.