Wazayuni wafanyia istihzai vitisho vya Trump dhidi ya Hamas
Gazeti la Kizayuni la Haaretz lilmefanyia istihzai vitisho vya Donald Trump dhidi ya Hamas na eneo zima la Asia Magharibi kwa sababu ya mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa HAMAS.
Donald Trump, rais mteule wa Marekani amedai kwamba kama mateka wa utawala wa Kizayuni hawataachiliwa huru huko Ghaza kabla ya yeye kuingia katika Ikulu ya White House tarehe 20 mwezi ujao wa Januari, basi "Mashariki ya Kati" yote itawaka moto.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limekejeli na kufanyia istihzai vitisho hivyo likisema kuwa, hivi sasa tayari moto unawaka Ghaza, ni moto gani mwingine ambao Trump amekusudia kuuwasha?
Katika ripoti iliyoandikwa na mwandishi wake Rachel Fink, gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kwa kejeli kwamba ni tabia ya Trump ya kutoa ahadi chapwa na kupenda kujifakharisha kwa mambo asiyofanya.
Gazeti hilo pia limeandika: "Ni kana kwamba kila mtu amesahau kuwa Trump ndiye aliyeahidi katika kampeni yake ya 2020 kwamba angeliilazimisha Mexico kutoa fedha za kujengwa ukuta katika mpaka wake na Marekani na daima amekuwa akiwaahidi Wamarekani kwamba angeboresha hali yao ya maisha lakini hafanyi hivyo.
Mwandishi huyo wa gazeti la Kizayuni la Haaretz pia amesema, wale waliopoteza kumbukumbu wanaweza kuamini ahadi za Trump lakini wakumbuke kuwa ni huyo huyo Trump ndiye aliyewaahidi Wamarekani kwamba angemaliza janga la UVIKO-19 na kuimarisha uchumi kuliko nchi nyingine yoyote lakini je, alifanya hivyo?
Siku chache zilizopita, Trump ametoa vitisho vya wazi dhidi ya Muqawama wa Palestina na kuunga mkono moja kwa moja jinai za utawala wa Kizayuni.