Afisa wa Hamas asema mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yameanza tena
Afisa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas amesema wapatanishi wa kimataifa wameanza tena mazungumzo na harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina na Israel kuhusu kusitisha mapigano Gaza.
Afisa huyo wa ofisi ya kisiasa ya Hamas alisema siku ya Ijumaa kwamba juhudi zimeanzishwa tena kwa lengo la kukomesha mauaji ya kimbari na kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.
Basem Naim ameliambia shirika la habari la Associated Press nchini Uturuki kwamba makubaliano ya kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel yaliyodumu kwa muda wa miezi 14 yanatarajiwa kufikiwa.
Amesema kuwa Hamas haijapokea pendekezo "imara" la kusitisha mapigano. Naim amesema Hamas inasisitiza kuhusu matakwa ya msingi ambayo iliwasilisha katika duru zilizopita za mazungumzo, ikiwa ni pamoja na usitishaji vita wa kudumu, kuondoka kabisa vikosi vya Israel kutoka Ukanda wa Gaza, na haki ya Wapalestina waliokimbia makazi yao huko Gaza kurejea makwao.
Lakini pia amesema kundi hilo la muqawama wa Palestina "liko tayari kulainisha msimamo" lakini tu katika utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kwenye ratiba ya kuondoka kwa wanajeshi wa Israel kutoka sehemu muhimu za Gaza.
Wakati wa duru ya awali ya mazungumzo mwezi Agosti, Israel ilidai kwamba baada ya kusitishwa mapigano yoyote, idumishe uwepo wa kijeshi katika 'mstari' wa Philadelphia, ambao ni eneo la kimkakati kwenye mpaka wa Gaza na Misri, na katika eneo la Netzarim.