Mabeberu wafanya njama za kuigawa vipandevipande Syria
Mmoja wa viongozi wa muungano wa Fat'h wa nchini Iraq amesema kuwa, kuna maelfu ya magaidi wametoroka jela nchini Syria na hiyo ni sehemu ya njama kubwa za madola ya kibeberu za kuligawa vipandevipande taifa hilo la Kiarabu.
Mtandao wa habari wa al Maaluma wa nchini Iraq umemnukuu Sadiq Abdullah, mmoja wa viongozi waandamizi wa muungano wa Fat'h wa nchi hiyo akisisitiza kuwa, maelfu ya magaidi hao waliotoroka jela nchini Syria ni raia wa nchi saba tofauti.
Amesema, hilo limetokea baada ya wapinzani wa serikali ya Syria kuvamia jela hizo. Ameongeza kuwa, hilo ni tishio kubwa kwa usalama wa nchi zote za eneo hili hasa Iraq.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa muungano wa Fat'h wa Iraq vilevile amesema kuwa, magenge ya kigaidi hayana kheri yoyote kwa nchi za eneo hili, yanatumika tu kama wenzo wa nchi za Magharibi wa kuzishinikiza nchi za ukanda huu. Amesema: Magenge hayo yanamiminiwa fedha na silaha kutoka kila upande ili yafanye jinai nchini Syria.
Aidha amesema, matukio ya Syria ni muendelezo wa njama kubwa ya kimataifa ya kuigawa vipandevipande na kudhoofisha taasisi rasmi za nchi hiyo ili kuzusha fitna za kikabila na kiitikadi na kusambaratisha safu za Waislamu na Muqawama.