Uungaji mkono wa Marekani kwa sera za kujipanua za Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119876-uungaji_mkono_wa_marekani_kwa_sera_za_kujipanua_za_wazayuni
Sambamba na kukaribia wakati wa kushika rasmi madaraka rais mteule wa Marekani Donald Trump, mipango na njama za Washington za kuunga mkono sera za kujipanua za utawala wa Kizayuni wa Israel nazo pia zimeongezeka.
(last modified 2024-12-08T09:03:57+00:00 )
Dec 08, 2024 09:03 UTC
  • Uungaji mkono wa Marekani kwa sera za kujipanua za Wazayuni

Sambamba na kukaribia wakati wa kushika rasmi madaraka rais mteule wa Marekani Donald Trump, mipango na njama za Washington za kuunga mkono sera za kujipanua za utawala wa Kizayuni wa Israel nazo pia zimeongezeka.

Katika wiki za karibuni, kuunga mkono mipango ya kujipanua na ya ukaliaji ardhi kwa mabavu ya Israel, imekuwa maudhui kuu inayofanyiwa kazi na washauri wa Trump na washirika wake wa karibu, na wamekuwa wakilizungumzia suala hilo katika nyanja tofauti. Moja ya nukta kuu ambazo washauri na washirika wengi wa karibu wa Trump wanaitilia mkazo ni kunyakuliwa na kuhodhiwa eneo lote la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
 
Katika msimamo wa karibuni zaidi kuonyeshwa na wapambe hao wa Trump, Tom Cotton, seneta wa chama cha Republican amependekeza mpango wa kubadilisha jina la Ukingo wa Magharibi. Katika mpango wake huo, Cotton ametaka jina la Kiyahudi la Ukingo wa Magharibi la Judea na Samaria liwe ndilo linalotumika katika hati na nyaraka zote rasmi za Marekani.
Cotton

Kabla ya hapo, Mike Huckabee, balozi mpya wa Marekani katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), naye pia alitamka kuwa, serikali ya Donald Trump iko tayari kuunga mkono mpango na mkakati wowote wa serikali ya Netanyahu wa kuuhodhi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kurasimishwa mamlaka ya utawala ya Israel katika eneo hilo.

Mpango wa kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel ni moja ya mihimili mikuu ya mpango wa kibaguzi uitwao "Muamala wa Karne", ambao ulitaka kuekelezwa na Marekani katika muhula uliopita wa urais wa Trump, na hivi sasa baadhi ya washauri wake wameibuka na kuzungumzia tena utekelezaji wake.

Ukweli ni kuwa, lobi ya ushawishi wa Israel ndani ya Marekani sasa hivi inahaha na kujaribu zaidi ya ilivyokuwa wakati mwingine wowote ule huko nyuma, kuvutia msukumo na uungaji mkono wa Trump; na inafanya kila njia kubadilisha hali ya mambo kwa manufaa ya Israel. Kukalia kwa mabavu ardhi nyingi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni moja ya matakwa muhimu zaidi ya lobi hiyo; suala ambalo halipingwi na Wapalestina na wapenzi wa Palestina pekee, lakini halikubaliki pia hata kwa mtazamo wa sheria za kimataifa.
Katika miaka ya karibuni, kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, Israel imeongeza kasi ya mchakato wa ujenzi wa vitongoji katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi na Baitul Muqaddas Mashariki kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa. Sambamba na hayo, tangu mwaka 2023, mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka uliomo kwenye baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu umelifanya kuwa sera rasmi, kwa kulitangaza hadharani na kulifuatilia kwa uzito mkubwa suala la kuuhodhi Ukingo wa Magharibi; ambapo vita vya Ghaza na hali ya sasa ya Wapalestina kwa upande mmoja, na mazingira ya kisiasa ya Marekani na kuchaguliwa Trump kwa upande mwingine, vimetoa fursa zaidi ya kutekelezwa mpango huo wa kupora na kughusubu ardhi hiyo.
Smotrich

Kuhusiana na suala hilo, Bezalel Smotrich, waziri wa fedha wa utawala wa Kizayuni amesema ana matumaini kuwa, kwa ushirikiano wa serikali mpya ya Marekani, fursa kubwa itapatikana ya kuufuta uendeshaji wa kiraia katika Ukingo wa Magharibi unaojumuisha pia Ukanda wa Ghaza. Smotrich amezungumzia pia mpango wa kutaifisha eka zipatazo 6,700 za ardhi ya Ukingo wa Magharibi, ambayo ni hatua kubwa zaidi kuchukuliwa tangu Makubaliano ya Oslo mwaka 1993. 

 
Ukweli ni kuwa, viongozi wa Israel sasa hivi wanafanya juu chini ili kutekeleza dhamira yao uvamizi, ukaliaji ardhi kwa mabavu na kujipanua katika Ukingo wa Magharibi. Kuhusiana na njama hiyo, harakati ya Hamas imesisitiza kuwa, sera ya upanuzi wa vitongoji na hujuma za walowezi dhidi ya miji na vijiji vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ni hatari kubwa kwa Wazayuni, kwa sababu kwa Muqawama na istiqama yao, wananchi wa Palestina wataishinda tu mipango ya Wazayuni ya kunyakua ardhi zao na kuwahamisha kwa nguvu katika makazi yao.
 
Kwa hiyo, hata kama kuchaguliwa kwa Trump kumezidi kuupa matumaini utawala wa Kizayuni ya kufanikisha sera zake za kivamizi, lakini historia inaonyesha kuwa wananchi wa Palestina wakiwa ndio wamiliki wa asili wa ardhi ya Palestina hawatasalimu amri katu kwa njama na sera za aina hiyo, na kama ilivyosisitiza Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ukingo wa Magharibi utabaki kuwa volkano ya mapinduzi na ghadhabu, hadi maghasibu watakapoangamizwa.../